Serikali imeielekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli( PURA) kuendelea kuvutia uwekezaji katika vitalu vilivyo wazi vya mafuta na gesi asilia ili kuongeza kiasi cha nishati hiyo nchini.
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ametoa maelekezo hayo Februari 19, 2025 Wilayani Morogoro, Mkoa wa Morogoro wakati akifungua kikao cha Baraza la wafanyakazi wa PURA kinacholenga kujadili masuala mbalimbali ikiwemo Mpango na Bajeti ya Taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26.
“Mkifanikiwa kuvutia uwekezaji katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi, nchi itaongeza ugunduzi wa rasilimali hiyo muhimu ikiwa ni pamoja na kuogeza futi za ujazo wa gesi inayopatikana nchini.
Pia mkiendelea kuvutia uwekezaji kupitia Duru ya Tano ya kunadi vitalu itakayozinduliwa mwezi Machi mwaka huu, pamoja na faida zilizopo, mtakuwa mmeendeleza jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuendelea kuifungua Tanzania kiuchumi na kuvutia uwekezaji Zaidi,” amesema Kapinga.
Amesema Wizara ya Nishati inatambua umuhimu wa tukio la Duru ya Tano ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini pamoja na kutambua kazi kubwa ambayo imeshafanyika kuelekea uzinduzi wa tukio hilo ambalo amesema kuwa ni muhimu katika
kuvutia uwekezaji zaidi katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini.
“Kwa muda mrefu sasa tumekuwa tukizungumzia ugunduzi wa futi za ujazo trilioni 57.54 pekee ni wakati sasa wa kufanya zaidi na zaidi ili tuweze kuongeza ugunduzi wa rasilimali hii muhimu kwa maendeleo ya Taifa,” amesisitiza Kapinga
Katika kikao hicho cha Baraza la wafanyakazi, ameupongeza uongozi wa PURA kwa kuendelea kuwashirikisha watumishi wake katika kujadili, kupanga na kupitisha mipango na Bajeti ya Taasisi kwenye Baraza la Wafanyakazi ikiwa ni utekelezaji pia wa Sheria ya Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Umma.