Serikali ya Tanzania na Canada imepanga kuwajengea uwezo wataalamu na wachimbaji wa madini nchini Tanzania katika matumizi ya teknolojia ya kisasa ya uchimbaji na uchenjuaji madini.
Hayo yameelezwa wakati wa mazungumzo baina ya Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada Ahmed Hussein na Waziri wa Madini wa Tanzania Anthony Mavundeyaliyofanyika Machi 04, 2025 Toronto, Canada na kuhudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Canada Joseph Sokoine pamoja na wataalamu wa Wizara zote mbili.
Akitoa maelezo ya awali, Waziri Ahmed Hussein ameipongeza Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Hassan kwa namna ambayo imeweka mazingira mazuri ya ukuaji wa sekta ya Madini nchini na kwamba Canada itaendelea kuimarisha uhusiano wake na Tanzania hasa katika eneo la kuwajengea uwezo wataalamu na wachimbaji madini kwenye matumizi sahihi ya teknolojia ya uchimbaji na uchenjuaji madini.
“Tumekuwa na miradi ya maendeleo ya elimu nchini Tamzania, hivyo kupitia vyuo vya mafunzo ya Ufundi itakuwa rahisi kuja na mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wananchi wa Tanzania, hasa wakina mama na vijana, kushiriki kikamilifu kwenye mnyororo mzima wa sekta ya madini,“ amesema Hussein.
Kwa upande wake, Waziri Mavunde ameishukuru nchi ya Canada kwa ushirikiano mkubwa inaoutoa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini na pia kubainisha uwepo wa Kampuni kubwa za Madini kutokea nchini Canada zimechochea kwa kiwango kikubwa maendeleo ya kiuchumi kupitia fursa mbalimbali zitokanazo na uwekezaji huo.
“Tanzania hivi sasa tuna programu yenye lengo la kuwezesha ushiriki kamilifu wa wakina mama na vijana kwenye sekta ya madini, hivyo kuwajengea uwezo wa kiujuzi kwenye mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya madini kutachochea kukua kwa kasi kwa sekta ya madini,” ameeleza Waziri Mavunde.