Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko amesema ataunda timu maalum itakayohusika na uchunguzi wa migodi yote nchini ikiwa ni pamoja na utambuzi wa aina ya madini yanayopatikana katika migodi iliyopo halmashauri ya wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro ili kuhakikisha wizi wa madini unakomeshwa nchini.
Akizungumza wakati wa ziara ya siku mbili mkoani Morogoro, Biteko amesema kuwa madini yote yaliyopo katika ardhi ya Tanzania ni mali ya watanzania na yanatakiwa kuwanufaisha watanzania.
Vilevile, Naibu Waziri huyo amefanya ziara ya kikazi katika kijiji cha Ipanko kilichopo katika wilaya ya Ulanga mkoani humo ambapo amedai kugundua kuwa baadhi ya wawekezaji wamekuwa wakiidanganya na kuiibia serikali kwa kutotoa ripoti sahihi juu ya mapato yao.
Akielezea suala la baadhi ya wawekezaji kutokuwa waaminifu, Biteko amesema haiwezekani muwekezaji akawekeza Sh. 42 bilioni na kuchangia madawati na mifuko ya saruji katika jamii kama mchango wake. Amewataka wawekezaji wote nchini kuchangia kulingana na kiasi ambacho wanawekeza.
Baadhi ya wananchi wamempongeza Naibu Waziri huyo kwa kufika kijijini hapo na kusikiliza kero zao wakiamini kuwa zitatafutiwa ufumbuzi wa kudumu.