Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein amewakaribisha wawekezaji pamoja na wafanyabiashara kutoka nchini Indonesia kufika Zanzibar kwa ajili ya kuwekeza na kufanya biashara. Dk. Shein amesema hayo wakati akizungumza na wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda wa Indonesia na kuongeza kuwa serikali inaboresha mazingira ili kuendelea kuwavuta zaidi wawekezaji.
Dk. Shein amewaambia wanajumuiya hao kuwa moja kati ya sababu ambazo Zanzibar inajivunia ni hali ya usalama, amani na utulivu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) Salum Khamis Nasssor ametaja baadhi ya sekta ambazo wawekezaji wanaweza kuanzisha miradi kuwa ni pamoja na kilimo, biashara, uvuvi, utalii, nishati pamoja na ujenzi wa miji mipya.
Vilevile katika mkutano huo, Dk. Shein ameeleza kuhusu jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali ili kuboresha sekta ya uvuvi ambapo ameeleza kuwa ujenzi wa bandari pamoja na viwanda vidogo vya samaki unaendelea.