Takribani Sh. 45 bilioni zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi (VETA) kwa mikoa ya Njombe, Geita, Rukwa na Simiyu. Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Peter Maduki amesema hayo kwa nyakati tofauti wakati wa hafla fupi ya kukabidhi maeneo ya ujenzi wa vyuo kwa mkoa wa Geita.
Maduki ameeleza kuwa ujenzi wa vyuo hivyo unalenga kutekeleza mkakati wa mamlaka hiyo wa kudahili wanachuo wapatao 700,000 ifikapo mwaka 2020 na kuongeza kuwa, serikali inafanya jitihada kubwa kuhakikisha vijana wanapata ujuzi stahiki, utakaowawezesha kuajiriwa au kujiajiri ili waweze kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi na kuhakikisha nchi inafikia uchumi wa kati mwaka 2025.
Chuo cha Veta mkoani Geita kina ukubwa wa hekta 27 na kitajengwa na kampuni ya Skywards Construction ya hapa nchini kwa mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kwa gharama ya Sh. 9.9 bilioni.
Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Geita, Gabriel Robert amemshukuru Rais Magufuli kwa kazi kubwa anayofanya kuboresha miundombinu mbalimbali nchini pamoja na ujenzi wa vyuo hivyo vya kisasa ambavyo vitawawezesha wananchi hususani vijana kupata ujuzi wa kujiajiri na kuwavutia wawekezaji.