Kampuni ya Kimataifa inayojishughulisha na masuala ya bima, Marsh imetoa dhamana yenye thamani ya Sh. 217 bilioni (takribani Dola za Marekani 95 milioni) kwa kampuni ya ujenzi ya Yapi Markezi Construction and Industry Inc. ili kuiwezesha kampuni hiyo kukamilisha mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) unaoendelea hapa nchini. Dhamana hiyo imewezeshwa kwa ushirikiano na taasisi ya African Trade Insurance Agency (ATI) inayojikita katika kutoa bima kwa shughuli za uwekezaji mkubwa barani Afrika.
“Ushirikiano wetu wa Marsh umetuwezesha kusimama kwenye moja ya vipaumbele vyetu vikuu ambavyo ni pamoja na kuwezesha kuongezeka kwa uwekezaji kwa nchi za kiafrika ambazo ni wanachama wa ATI. Uwekezaji mkubwa kama huu unaweza kufanyika kama kunakuwepo na dhamana mahususi ya bima. ATI imewezesha uwekezaji wa zaidi ya Dola za kimarekani bilioni moja kwa hapa Tanzania katika miaka ya hivi karibuni. Mradi utawezesha Tanzania kuwa na reli ya kisasa ambayo ni muhimu katika maendeleo ya watu wake”. Amefafanua Mwakilishi wa ATI Tanzania, Tusekile Kibonde.
Kampuni ya Yapi Markezi ilipewa mkataba wa ujenzi wa SGR na serikali kupitia Kampuni Hodhi ya Mali za Reli (RAHCO). Ujenzi wa reli hiyo ya kisasa utagharimu Dola za kimarekani 1.25 bilioni na ukikamilika, reli hiyo yenye umbali wa kilomita 300 itakuwa na uwezo wa kusafirisha tani milioni 17 kwa mwaka.