Naibu Kamishna wa Kodi za Ndani kutoka Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) Abdul Zuberi amesema mamlaka hiyo inawataka mawakala wote wa forodha kuhakakisha wanahakiki namba zao za Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza na wakati huo huo, kuisaidia mamlaka hiyo kukusanya mapato. Zuberi amesema hayo katika semina iliyowakutanisha na makampuni ya mawakala wa forodha, semina ambayo imejadili masuala mbalimbali yanayohusu kodi na ushuru wa forodha.
Naibu Kamishna huyo amesema kuwa, mawakala hao wanapaswa kuhakiki TIN zao kutokana na baadhi ya watu kuwa na TIN zaidi ya moja, hali ambayo amedai kuwa, inawapa changamoto ya kutambua idadi ya mawakala wanaotakiwa kulipa kodi.
“Kuna watu wana TIN zaidi ya moja wanazitumia bila kufanyiwa uhakiki na wengine wanazifanyia udanganyifu inatupa tabu kuwatamabua hivyo ni vema mkazifanyia uhakiki”. Ameeleza Naibu Kamishna huyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha (TAFA) Frank Kamugisha ametoa wito kwa mamlaka hiyo kujenga utaratibu maalum wa kukutana nao kuzungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.