Naibu Waziri wa Kilimo, Omar Mgumba ametoa ufafanuzi kufuatia madai ya watu mbalimbali kuwa, korosho inanunuliwa chini ya Sh. 3,300 ambayo ni kinyume na agizo lililotolewa na Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli.
Akiwa bungeni Dodoma akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe ambaye alihoji kwanini wanunuzi wa korosho wamekiuka agizo la moja kwa moja la Rais Magufuli na kulipa chini ya kiwango tofauti na walivyoelekezwa, Mgumba ameeleza kuwa korosho inanunuliwa kwa Sh. 3,300 kwa kilo moja na kwamba maagizo ya Rais hayajakiukwa. Mgumba amesema zao hilo hununuliwa kwa kiasi cha Sh. 3,300 kwa korosho daraja la kwanza, huku daraja la pili likinunuliwa kwa Sh. 2,640.