Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi amewataka wafanyabiashara hasa wa mitandaoni kujisajili ndani ya siku tisini. Hapi amesema hayo baada ya kupokea ripoti ya ugawaji wa vitambulisho katika mkoa huo, ipoti ambayo inaonyesha kuwa, hadi sasa vitambulisho vya awali 25,000 vimeshawafikia wafanyabiashara wadogo 9,000. Mkuu huyo wa mkoa amewasisitiza wajasiriamali kupata vitambulisho hivyo kwa faida yao na pia kwa faida ya nchi kwa ujumla.
“Wanaouza nguo, keki, vyakula, bidhaa za tiba za jadi na biashara yoyote ile mkoani kwetu kupitia mitandao ya kijamii, katika simu za mikononi na vifaa vingine vinavyotumia tekinolojia ya kisasa ya mawasiliano watatafutwa ili wasajiliwe katika moja ya mifumo hiyo”. Amesema Hapi.
Aidha, Mkuu huyo ameitaja mifumo hiyo kuwa ni ule wa leseni za biashara zinazotambuliwa na Halmashauri inayopitia namba za utambulisho wa mlipa kodi (TIN) katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na wa vitambulisho vya wajasiliamali wadogo vilivyoanza kutolewa hivi karibuni na Rais John Magufuli.
Hapi pia ameongeza kuwa, Tanzania itajengwa kwa kupitia mchango wa watanzania. Hivyo mpango wa kuwaweka wajasiriamali katika ulipaji kodi unatakiwa kuwahusisha hata wale wanaoendesha VICOBA.