Home Uncategorized Kamati ya kitaifa mradi wa BEAR II yakutana Dar

Kamati ya kitaifa mradi wa BEAR II yakutana Dar

0 comment 109 views

Kamati ya kitaifa ya mradi mkubwa wa kuboresha elimu ya ufundi kwa lengo la kuwajengea uwezo vijana katika ajira mbalimbali sokoni na binafsi unaofadhiliwa na Korea Kusini kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) imekutana jijini Dar es salaam kupitia pamoja na mambo mengine ratiba ya utekelezaji wa mradi huo.

Ofisa wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Jennifer Kotta akitambulisha meza kuu wakati wa kikao cha kamati ya kitaifa cha kupitia ratiba ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa kuboresha elimu ya ufundi (BEAR II) kwa lengo la kuwajengea uwezo vijana katika ajira mbalimbali sokoni na binafsi unaofadhiliwa na Korea Kusini kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) uliofanyika mwishoni mwa wiki Hoteli ya Protea Courtyard jijini Dar es Salaam.

Mradi huo ambao unajulikana kama The Better Education for Africa’s Rise, (BEAR) unaendeshwa pia katika nchi za Madagascar, Ethiopia, Uganda na Kenya na ni sehemu ya mradi wa kimataifa wa elimu maarufu kama Education 2030 Agenda , moja ya malengo ya maendeleo endelevu ya kimataifa, lengo namba nne, na unafadhiliwa na Korea kusini kwa dola za Marekani milioni 10.

Akizungumza Mkuu wa Kitengo cha Elimu katika Shirika la UNESCO nchini, Faith Shayo alisema kwamba mradi huo unaotarajiwa kukamilika 2021 umelenga kuboresha utaalamu na kuwezesha vijana kuajiriwa au kujiajiri wenyewe kwa kuangalia fursa zilizopo kwa kadri ya mahitaji ya nchi.

Mkuu wa Kitengo cha Elimu katika Shirika la UNESCO nchini, Faith Shayo akifafanua jambo wakati wa kikao cha kamati ya kitaifa cha kupitia ratiba ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa kuboresha elimu ya ufundi (BEAR II) kwa lengo la kuwajengea uwezo vijana katika ajira mbalimbali sokoni na binafsi unaofadhiliwa na Korea Kusini kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) uliofanyika mwishoni mwa wiki Hoteli ya Protea Courtyard jijini Dar es Salaam.

Mradi huo ambao sasa unaingia katika awamu ya pili,na hivyo kujulikana kama BEAR ll ulianza mwaka 2017 na unatarajiwa kutekelezwa hadi 2021, kazi kubwa ikiwa ni kuwezesha vijana kupata ajira zenye staha na pia kujenga uwezo wa kujiajiri kwa vijana kwa kuboresha mifumo na ufundishaji wa elimu ya ufundi stadi.

Alisema nchini Ethiopia, mradi huu umejikita zaidi katika sekta ya uchakataji mazao ya kilimo; Kenya ipo uhifadhi wa mazingira, utengenezaji wa nafasi za kazi za kutunza mazingira; Madagascar ipo kwenye viwanda vya nguo; Uganda imejikita katika menejimenti ya mazao baada ya kuvunwa na uchakataji wa bidhaa za chakula zinazotokana na kilimo wakati nchini Tanzania imejikita katika biashara za mazao ya kilimo na ubunifu.

“Tunatarajia baada ya kukamilika kwa mradi huu kutakuwepo na maendeleo makubwa katika mifumo ya elimu na ufundishaji wa elimu ya ufundi stadi nchini Tanzania,” alisema Shayo wakati akiwasilisha mpango kazi unaotakiwa kufuatwa katika kikao hicho cha kitaifa mwishoni mwa wiki.

Alisema kwamba BEAR II inatekelezwa kwa kuzingatia fundisho lililopatikana kwenye awamu ya kwanza iliyoanza 2011-2016 ambayo ilisaidia kunoa mifumo ya ufundi stadi na ufundishaji wake katika nchi 5 za Jumuiya ya Uchumi Kusini mwa Afrika (SADC) za Botswana, DR Congo, Malawi, Namibia, na Zambia.

BEAR II ambayo inajengwa kwa kuzingatia vipaumbele vya kila taifa, inaingilia maeneo matatu ili kufanya mafunzo ya ufundi kuwa na maana zaidi kwa kuzingatia mahitaji ya kiuchumi na soko; kuboresha zaidi programu zinazoambatana na elimu hiyo na pia kuboresha uelewa na matamanio ya elimu ya ufundi miongoni mwa vijana.

Mradi wa BEAR kwa kila nchi unafanywa kwa ushirikiano kati ya wadau mbalimbali wa elimu, wizara ya elimu na serikali za nchi husika.

Imeelezwa kuwa kazi kubwa ya UNESCO katika mradi huo ni ya menejimenti, ufuatiliaji na ufanyaji wa tathmini na serikali ya Korea yenyewe itatengeneza mfumo wa ufuatiliaji na kufadhili utekelezaji wake.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter