Benki ya Maendeleo ya TIB imetoa mafunzo ya namna ya kuandika andiko la uombaji mikopo kwa watumishi 160 katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Shinyanga. Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa watumishi hao (wahasibu, wahandisi, maofisa maendeleo ya jamii, maofisa ugavi na maofisa mipango) hasa pale Halmashauri zao zinapokuwa zikihitaji mikopo ya kimaendeleo na ruzuku kutoka serikalini.
“Niwaombe mtumie fursa hii kujifunza, miradi mingi ya Halmashauri huwa tunaamini wapo wataalamu, lakini tumieni fursa hii kufanya mabadiliko”. Amesema Kwitega.
Mkurugenzi wa Mipango, Mikakati na Mawasiliano wa TIB, Patrick Mongella, amewataka watumishi hao kutopoteza muda wao kuandika nyaraka za mikopo zenye maneno mengi yasiyo na msingi na badala yake kuandika vitu muhimu ambavyo vitawasaidia kupata mikopo hiyo. Mongella ametaja baadhi ya miradi ambayo wanaweza kujipatia mikopo kwa kuandika nyaraka stahiki kuwa miradi ya vituo vya mabasi, maeneo ya viwanda, uhakiki wa viwanja na ardhi.
Mafunzo hayo yamewanufaisha watumishi 300 katika mikoa ya Mbeya na Mwanza ambapo yalifanyika mwaka 2018.