Home BIASHARAUWEKEZAJI Serikali yaandaa mpango maalum kuimarisha wawekezaji

Serikali yaandaa mpango maalum kuimarisha wawekezaji

0 comment 100 views

Na Grace Semfuko-MAELEZO

Serikali inaandaa mpango maalum wa kuimarisha na kuongeza wawekezaji katika sekta mbalimbali ikiwepo ya mifugo na kilimo ili kuongeza upatikanaji wa nyama, siagi na maziwa pamoja na chakula nchini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anaeshughulikia Uwekezaji Angellah Kairuki amesema mpango huo unaanza na kuzungumza na wawekezaji katika nchi mbalimbali duniani ambao wana uwakilishi wa kibalozi nchini Tanzania.

Kairuki aliyasema hayo ofisini kwake jijini Dar es Salaam mara baada ya kufanya mazungumzo na mabalozi watatu wanaoziwakilisha nchi zao akiwepo Balozi wa Afrika Kusini Bw. Thamsanqa Dennis Mseleku, Balozi wa Ireland Bw Paul Sharlock na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Bi Imni Paterson ambao kwa nyakati tofauti wamemweleza Waziri kuwa wamekuwa na mpango madhubuti wa kuongeza wawekezaji binafsi ili kuinua uchumi na kuongeza ufanisi wa bidhaa za viwanda.

Kairuki alisema Serikali inaandaa mikutano mikubwa na wawekezaji wa nchi hizo Jijini Dar es Salaam ambapo ataanza na wawekezaji wa China utakaofanyika April 17 mwaka huu ukihusisha pia taasisi mbalimbali za serikali zinazosaidia uwekezaji ili kuangalia fursa, kushauriana na kusikiliza changamoto za uwekezaji nchini.

Kwa upande wake Balozi wa Ireland nchini Tanzania Bw. Paul Sharlok alisema nchi yake inaendelea kuhamasisha wawekezaji na kutangaza vivutio vyilivyopo Tanzania ambapo katika mkutano mkubwa wa kiuchumi wa Ireland na Afrika unaofanyika mara moja kwa miaka miwili kwa mwaka jana walipendekeza kuwekeza kwenye sekta ya kilimo biashara na kuwaunganisha wawekezaji wa Ireland na Tanzania katika kufanya kazi pamoja.

“Sisi Ireland tuna mpango maalum kuhusu uchumi wa Afrika, kila baada ya miaka miwili tunakuwa na mkutano mkubwa wa kiuchumi wa Ireland na Afrika, mwaka jana tulizungumzia kilimo biashara na tuliweza kuwaunganisha wafanyabiashara wengi wa Tanzania, mwakani tutafanya mkutano huo natumaini sekta binafsi na Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC watashiriki”. Alisema Balozi Sharlock.

Naye Balozi wa Marekani nchini Tanzania Imni Paterson alisema kwa muda mrefu Marekani imekuwa na mikakati mingi ya kiuchumi kuhusu Tanzania, wataiendeleza mikakati hiyo na pia wataanzaa mkutano wa pamoja baina ya Wizara ya Uwekezaji na wawekezaji wa kimarekani ili kupata majadiliano ambayo yatasaidia pande zote.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter