Home FEDHA Dodoma, Dsm zang’aa ukusanyaji mapato

Dodoma, Dsm zang’aa ukusanyaji mapato

0 comment 108 views

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mtaa (TAMISEMI), Selemani Jafo amesema kufikia robo tatu ya mwaka wa fedha 2018/2019, Halmashauri hapa nchini zimekusanya mapato ya Sh. 449.8 bilioni (sawa na 61%) kutoka vyanzo vya ndani. Jafo amesema hayo jijini Dodoma wakati akitoa taarifa za makusanyo kuanzia Juni 2018 hadi Machi mwaka huu. Katika maelezo yake, Waziri huyo ametaja Halmashauri ya jiji la Dar es salaam na Dodoma kuongoza kwenye ukusanyaji wa mapato ghafi.

Halmashauri nyingine zilizofanya vizuri kwa asilimia ya mapato ya ndani ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi (113%), Geita (109%), Wanging’ombe (105%), Kilolo (103%) na Sumbawanga (92%). Zilizofanya vizuri kwa wingi wa mapato ni Dodoma (Sh. 49.9 bilioni), Ilala (Sh. 44.8 bilioni), Kinondoni (Sh. 23.5 bilioni), Temeke (Sh. 20.6 bilioni) na Arusha (Sh. 12.5 bilioni) wakati zilizofanya vibaya zikiwa ni Madaba (Sh. 293.7 milioni), Newala (Sh.268.3 milioni), Kakonko (Sh. 238.6 milioni), Buhigwe (Sh. 177.3 milioni) na Momba (Sh. 170.4 milioni).

Mikoa iliyofanya vizuri kwa upande wa asilimia ya mapato ya ndani ni Iringa (77%), Geita (73%), Dar es salaam (72%), Songwe na Dodoma (68%) wakati iliyofanya vibaya kwa kundi hili ni Shinyanga (46%), Katavi (43%), Mtwara (26%), Kigoma na Lindi (42%).

“Katika kigezo cha pato ghafi kwa Halmashauri za mji, Geita inaongoza baada ya kukusanya Sh. Bilioni 5.9 na Halmashauri ya Mji wa Nanyamba imekuwa ya mwisho ikiwa imekusanya Sh. 293.9 milioni”. Amesema Waziri huyo.

Kwa upande wa makisio, Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga imeongoza kwa kukusanya takribani 92% huku Lindi ikishika nafasi mkia baada ya makusanyo yake kufikia 23% pekee. Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imeongoza kwa mapato ghafi baada ya kukusanya Sh. 50 bilioni na Tanga imeshika nafasi ya mwisho kwa kukusanya Sh. 8.7 bilioni.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter