Home AJIRA Jinsi ya kuandika CV

Jinsi ya kuandika CV

0 comment 279 views

Mara nyingi nafasi za kazi zinapotangazwa, utakuta kwenye vigezo au masharti wanaelekeza kwamba muombaji anapaswa kuambatanisha wasifu wa ujuzi (Curriculum Vitae au maarufu zaidi kama CV). Wasifu ni moja ya nyaraka ambazo waajiri huangalia na kuamua kutoa au kutotoa ajira.

Yafuatayo ni mambo muhimu unayotakiwa kuzingatia unapoandaa Wasifu (CV)

1. Taarifa ya mawasiliano

Inafaa kuweka taarifa zako  za mawasiliano kama kichwa cha habari, hii itamsaidia mtu anayekuajiri kuzipata kwa haraka zaidi. Andika jina lako, namba ya simu, barua pepe na taarifa nyingine ambazo unafikiri ni muhimu mwajiri kujua na kuweza kukufikia kwa haraka.

Mfano: Jina: Mary Anne Paul Namba ya Simu: 0777 111 777 Barua Pepe: Marypaul@gmail.com

2. Taarifa binafsi

Hapa unaelezea kwa kifupi tu mwaka wako wa kuzaliwa, jinsia, uraia pamoja na lugha.

Mfano: Mwaka wa kuzaliwa: 7/9/2000 Jinsia: Kike Uraia: Mtanzania Lugha: Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa

3. Elimu

Hapa unatakiwa utaje elimu uliyo nayo, na sehemu uliyosoma. Kuna wengine hupendelea kuweka na miaka waliyomaliza elimu hiyo lakini ni muhimu kuwa na uhakika wa mwaka huo ili usimchanganye muajiri kama akitaka kujua zaidi kuhusu elimu yako.

Mfano: Elimu ya Chuo Kikuu: Shahada ya Uchumi- Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (2017)

Elimu ya Sekondari (5&6): HGE- St. Marian Secondary school (2015)

4. Uzoefu wa kazi

Katika kipengele hiki ni muhimu kuwa mkweli kwani waajiri wengi hufuatilia kwa makini, hivyo elezea kama umewahi kufanya kazi sehemu nyingine na weka wazi majukumu uliyokuwa nayo

Mfano: Kazi:  Upishi- Savanna Lounge (Machi 2016- hadi sasa)

Majukumu: Kupika chakula cha mchana, kuosha vyombo, kusafisha jiko, kuwahudumia wateja n.k.

5. Ujuzi

Ni muhimu muajiri wako afahamu kama una ujuzi zaidi ya kufanya kazi ulizowahi kufanya na kazi hiyo ambayo unahitaji. Hivyo kama una ujuzi zaidi, eleza kwenye wasifu wako kwani kulingana na kazi unayoenda kuomba, unaweza kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kuajiriwa.

6. Wadhamini

Hawa pia huwa muhimu katika wasifu wako kwa sababu ili muajiri aweze kuhakikisha. Kwa mfano kuhusu kazi ulizoandika kuwa umewahi kufanya, atahitaji kuongea na watu ambao watamuhakikishia kuwa ulichoandika ni sahihi. Unachotakiwa kufahamu ni kwamba wadhamini hawatakiwi kuwa wazazi au ndugu zako hivyo unashauriwa kuandika watu kama waajiri wako wa zamani au walimu wako chuoni.

Wakati unaandaa wasifu wako, ni vizuri kutengeneza jedwali ili iwe rahisi kwa mwajiri na pia kufanya hivyo huonyesha umakini wako katika masuala ya muhimu kama kazi. Mara nyingi wasifu huandikwa kwa lugha ya Kiingereza.

 

 

 

Tags:

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter