Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amesema inapaswa kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya visiwa hivyo na Brazil kwani wamekuwa wakishirikiana katika masuala mbalimbali ya maendeleo. Dk. Shein amesema hayo Ikulu Zanzibar wakati akizungumza na Balozi wa Brazil Antonio Augusto Cesar na kumhakikishia kuwa Tanzania na Zanzibar zimejipanga kuleta maendeleo makubwa kutokana na uwepo wa viongozi imara, hali ambayo imedumisha muungano kwa miaka takribani 55.
“Leo hii ni miaka 55 tangu nchi hizi kuungana, Muungano umebaki imara. Nchi nyingi zimejaribu kufanya hivyo, lakini zimeshindwa”. Amesema Rais huyo.
Pamoja na hayo, Dk. Shein amesema kuwa Zanzibar ambayo hapo awali ilikuwa ikitegemea karafuu pekee kukuza uchumi ina vivutio mbalimbali vya utalii kupitia uchumi wa bahari (Blue Economy) na kueleza kuwa, wanalenga kuwavutia zaidi wawekezaji kutoka Brazil ili kuendelea kuimarisha uchumi sio tu kupitia utalii bali kwenye sekta mbalimbali.
Kwa upande wake, Balozi Cesar amemueleza Rais Shein kuwa taifa lake linachukua hatua mbalimbali ili kuleta maendeleo ya kiuchumi, kisiasa pamoja na kijamii. Amemhakikishia Rais huyo kuwa Brazil itaendelea kutoa ushirikiano kwa Zanzibar.