Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema sekta ya kilimo inakumbwa na changamoto kubwa ya hasara katika uwekezaji hivyo Wizara hiyo kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo (DP), wameanza mchakato wa kuanzisha Bima ya Mazao (BM). Hasunga ameeleza hayo bungeni Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Kilimo na kuongeza kuwa changamoto mbalimbali kama vile mafuriko, ukame, wadudu waharibifu na magonjwa zimesababisha taasisi za kifedha kutoipa sekta ya kilimo kipaumbele kwenye suala zima la utoaji mikopo.
“Katika kukabiliana na changamoto hizo, nchi nyingi duniani zimeanza na kutekeleza mfumo wa bima ya mazao”. Amesema Waziri huyo.
Pamoja na hayo, Hasunga amesema uwepo wa bima ya mazao utasaidia wakulima kulipwa fidia pale hasara inapotokea na vilevile itarahisisha upatikanaji wa mikopo kwenye taasisi mbalimbali. Aidha, Waziri huyo ameeleza kuwa tayari vikao baina ya Wizara ya Kilimo na wadau kwa ajili ya kuandaa utaratibu wa bima hiyo kwa kuanza na mazao machache katika baadhi ya maeneo vimeshafanyika huku maandalizi yakiendelea ili angalau kuwepo na aina mbili za mifumo ya bima ya mazao inayoweza kutumika katika mwaka 2019/20.