Home BIASHARAUWEKEZAJI Japan na Tanzania kuendelea kushirikiana

Japan na Tanzania kuendelea kushirikiana

0 comment 115 views

 

Na Mwandishi wetu

Baada ya kufanya mazungumzo na Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje ambaye ni mwakilishi wa wabunge wa Japan kwenye masuala ya Afrika katika bunge la nchi hiyo,  Ichiro Aisawa, Rais John Pombe Magufuli ameshukuru serikali ya Japan kwa kushiriki miradi mikubwa ya maendeleo hasa ya miundombinu hapa nchini.

Taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari imesema mbunge huyo wa Japan ametembelea mradi wa barabara za juu (Flyover) Tazara na ule wa gesi wa Kinyerezi ambayo inajengwa na kampuni za Japan, na baadae kumhakikishia Rais Magufuli kwamba kampuni hizo zitafanya kazi nzuri na kumaliza miradi hiyo kwa wakati.

Baada ya kumaliza  ziara hiyo, Aisawa alishuhudia foleni za barabarani jijini hapa na kusema Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania ili kuboresha miundombinu katika jiji la Dar es salaam na kuahidi atazungumza na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe ili kusaidia Tanzania na changamoto ya foleni.

Naye Rais Magufuli amemshukuru kwa kutembelea nchi yetu na amesema Japan imejitolea kwa kiasi kikubwa katika shughuli za maendeleo na kwamba Tanzania itaendelea kushirikiana nayo katika masuala mbalimbali.

Japan imetoa fedha kuwezesha miradi mbalimbali jijini Dar es salaam. Baadhi ya miradi hiyo ni upanuzi wa barabara ya Mwenge-Morocco ambayo itawezesha njia hiyo kuwa na barabara nane, barabara ya Bendera tatu hadi Kamata, ujenzi wa barabara ya Tazara na ujenzi wa daraja la Gerezani njia nne.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter