Na Mwandishi wetu
Mamia ya wafanyabiashara wa soko la Sido jijini Mbeya wamepoteza biashara zao baada ya soko hilo kuteketea kwa moto ambapo ulianza katika banda moja la kuuzia nafaka na kasha kusambaa kwa kasisehemu nyingine sokoni hapo huku jitihada za kuzima moto huo zikigonga mwamba kutokana na ubovu wa miundombinu ya ndani ya soko hilo ambayo ilisababisha vikosi vya zimamoto na uhamiaji kushindwa kufika eneo la tukio kwa wakati.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amesema amesikitishwa na kushitushwa na tukio hilo na kuamuru vikosi vya zimamoto na uokoaji kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini nini kimesababisha moto huo na baadaye hatua zaidi zitachukuliwa, kwani hii ni mara ya nne kwa soko kuungua Mbeya tangu mwaka 2006.
Soko hilo lilikuwa na maduka na vibanda zaidi ya 3000 vya biashara na wafanyabiashara walioathirika na tukio hilo wameomba uchunguzi ufanyike ili kubaini undani wa matukio haya kwani yanatokea jijini humo tu. Naye Katibu wa soko hilo Lainus Ngogo amesema ni maeneo ya biashara 140 tu ambayo yamenusurika katika maafa haya huku moto huo ukileta hasara kubwa kwa wafanyabiashara.