Home AJIRA Vikwazo vya kuajiriwa na wazazi

Vikwazo vya kuajiriwa na wazazi

0 comment 107 views

Sio kila mtu hupitia kashkash za kutafuta kazi baada ya kuhitimu. Kuna watu ambao wamekuwa wakiandaliwa kufanya kazi katika biashara au kampuni ya familia. Kadri siku zinavyokwenda suala la ajira linaendelea kuwa gumu na ndio maana vijana wanashauriwa kujiajiri kuliko kusubiria ajira, hivyo ikiwa mtu amepata fursa ya kufanya kazi katika kampuni ya familia si rahisi kukataa kwani mamilioni ya watu wanatamani kupata fursa hiyo.

Hakuna kazi iliyo kamilifu, hivyo hata katika biashara ya familia kutakuwepo na mazuri na mabaya. Kabla hujafanya maamuzi ya kufanya/kutokufanya kazi katika kampuni au biashara ya familia zingatia vikwazo vifuatavyo:

Kukosa heshima. Hata kama unasifa zinazostahili katika kazi uliyopata katika kampuni ya familia. Siku zote wafanyakazi wengine, washirika na hata wateja watafikiria kuwa umepata kazi hiyo kwa sababu wewe ni mtoto wa mmiliki wa biashara au kampuni husika. Hivyo itakuwa si rahisi kupata heshima unayostahili. Utaonekana kuwa unapendelewa zaidi ya watu wengine hata kama haiko hivyo, hali ambayo inaweza kusababisha chuki kazini.

Migogoro. Ni jambo moja kuishi na familia yako nyumbani na ni jambo jingine kufanya kazi na familia yako. kufanya kazi na wanafamilia kunaweza kupelekea migogoro kwasababu wote mnajuana vizuri sana hivyo  ni vigumu kutofautisha maswala ya ofisi na binafsi. Ndio maana katika biashara au kampuni nyingi wanakataza mahusiano binafsi kati ya bosi na waajiriwa ili kuepusha kufanya maamuzi kutokana na hisia kwasababu kwa kufanya hivyo inaweza kuathiri familia na kampuni kwa ujumla.

Sio rahisi kuchangamkia fursa nyingine. Kwa kufanya kazi na familia huwa inakuwa si rahisi kuchangamkia fursa mbalimbali zenye maslahi zaidi kwa sababu siku zote ni muhimu kushikamana na familia ili kupata maendeleo zaidi. Hivyo itakuwa ngumu kuondoka na kwenda kuwafaidisha watu wengine ili hali familia yako inakuhitaji. Pia kitendo cha wazazi wako kukusomesha na kukufanya ufike hapo ulipo ni moja ya vitu ambavyo vitakufanya uone kwamba hakuna umuhimu wa kwenda sehemu nyingine wakati wazazi wako ndio wamekufanya ufike hapo ulipo.

Mapito. Kila kitu kinachotokea katika kampuni au biashara ya familia lazima kitakugusa wewe binafsi kama mwanafamilia na hisia zako pia zitaguswa kuliko ukifanya kazi katika kampuni nyingine inayomilikiwa na watu wengine. Hivyo faida na hasara zitakufanya uwe na hisia mbalimbali na wazazi wako wanaweza kuwa katika wakati mgumu ikiwa mambo hayaendi sawa (utahusika pia) ikiwa mambo yanakwenda vizuri basi Na wazazi nao watajivunia na kukuhakikishia kuwa ulifanya maamuzi sahihi kufanya nao kazi. Hivyo ni muhimu kujua kama uko dhaifu au imara katika mapito yoyote yanayoweza kutokea katika kampuni au biashara ya familia.

Mawazo yako yanaweza yasitiliwe maanani. Siku zote hata uwe umekua kiasi gani mzazi wako atakuchukulia kama mtoto wake mdogo. Hivyo kwa kufanya kazi na wazazi wako si kila wazo utakalotoa litatiliwa mkazo au maanani kama ambavyo mawazo ya wafanyaazi wengine yatakavyosikilizwa. Hiyo inaweza kukupelekea kuwa na hasira, hivyo ni muhimu kujua jinsi utakavyokabiliana na wazazi wako ikiwa jambo hili litatokea kabla hujakubali kufanya nao kazi.

Wakati wa familia, muda wa biashara/kazi. Kufanya kazi na wazazi wako humaanisha kuwa kila wakati lazima mada kuhusu kazi au biashara zitaongelewa. Kwa mfano muda wa kula lazima mazungumzo ya biashara yataanzishwa, hii inaweza kuleta shida katika uhusiano baina ya familia. Na inaweza kuonekana kuwa siku zinavyozidi kwena unapoteza uhusiano binafsi baina yako na familia yako kwa ujumla kwa sababu wameelekeza kila kitu katika biashara kuliko masuala binafsi.

Kwa ujumla changamoto si nyingi kama faida ikiwa unataka kufanya kazi katika biashara au kampuni ya familia. Jambo la msingi ni kuhakikisha kunakuwepo na mawasiliano ya wazi baina yako, wazazi na wafanyakazi wengine ili kila kitu kiweze kwenda sawa.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter