Home FEDHAMIKOPO Makosa ya kuepuka wakati wa kulipa deni

Makosa ya kuepuka wakati wa kulipa deni

0 comment 115 views

Kulipa madeni ni njia moja wapo ya kuboresha hali yako ya kifedha, Kwasababu unakuwa huna jukumu la kulipa madeni hayo pamoja na riba kwa watu au taasisi iliyokukopesha. Pia kwa kulipa madeni inakuwa rahisi kukopeshwa tena kwasababu taasisi au watu binafsi huwaamini zaidi watu wenye historia ya kukopa na kulipa madeni kuliko wale watu wasio na historia ya ukopaji au wale wenye historia ya kukopa na kutokurudisha fedha walizokopa.

Sawa kulipa deni ni muhimu lakini mara nyingi huwa si rahisi hasa ikiwa makosa yatafanyika wakati wa mchakato huo. Hivyo yafuatayo ni baadhi ya makosa ambayo unatakiwa kuhakikisha unayaepuka wakati wa kulipa deni ili kuwa na historia nzuri ya ukopaji na mtiririko mzuri wa fedha zako:

Kutokuwa na mpango wa malipo

Ni muhimu kujiwekea malengo ya wazi na mpango maalum wa jinsi utashughulikia mkopo wako na kuulipa kadri ya makubaliano baina  yako na mkopeshaji. Kwamfano unaweza kuamua ni madeni yapi yanatakiwa kuanza kulipwa mapema, au unaweza kuamua kulipa madeni yenye viwango vya juu vya riba ili kuepukana na gharama ikiwa itatokea utachelewa kuyalipa madeni hayo. Vilevile ni muhimu kuweka bajeti, kupunguza matumizi na kuamua ni kiasi gani unaweza kumudu kulipa kila mwezi, pia hakikisha unajua unadaiwa kiasi gani kwa ujumla ili kurahisisha kutengeneza mpango madhubuti wa kulipa madeni yako.

Kulipa kidogo kidogo kwa wakati mmoja

Kuna baadhi ya watu hupenda kulipa fedha kidogo kidogo kwa watu na taasisi zote zinazowadai bila kujua njia hiyo inaweza kuchukua muda mrefu kukamilisha malipo yote ya madeni yao na kwa namna moja au nyingine muhusika anaweza kukata tamaa kwasababu madeni yatakuwa yanaonekana kama hayaishi.

Badala yake, jitahidi kutumia fedha kidogo katika matumizi na bili, halafu fedha zinazobaki elekeza katika mkopo mmoja hadi utakapoumaliza mkopo huo unaweza kuelekeza fedha zako katika mkopo mwingine hadi utakavyomaliza mikopo yako yote.

Kutokufuatilia maendeleo yako

Kufuatilia juhudi zako za ulipaji wa madeni ni muhimu kwasababu kadri deni linavyoendelea kupungua utahamasishwa zaidi kulilipa deni hilo hadi liishe kabisa. Kwamfano unaweza kuhamasika kutafuta kazi nyingine ya ziada ili kuweza kupata fedha zaidi na kulilipa deni hilo. Hivyo kama haufatilii maendeleo  yako ya mkopo ni vyema kuanza sasa hasa kama unataka kuboresho mwenendo wako wa kifedha.

Kutokuwa na mfuko wa dharura

Unaweza kuona hakuna umuhimu wa kuwa na mfuko wa dharura katika kipindi ambacho umejikita kuyalipa madeni yako lakini si sahihi kuwa na mtizamo huo. Kwasababu kutokuwa na mfuko wa dharura kunawez kukusababisha ukope tena ikiwa jambo linalohusu fedha likatokea ghafla. Hivyo kama unafanya maendeleo kwenye ulipaji wa madeni ni vyema kuweka akiba ya fedha ili ziweze kukusaidia katika matatizo ya ghafla.

Kuendelea kukopa zaidi

Kuwa  na mfuko wa dharura ni muhimu ili kujiepusha na madeni zaidi- lakini matumizi makubwa, kutokuwa na bajeti,kunaweza kukusababisha uendelee kukopa ili kuweza kulipia matumizi hayo ambayo mara nyingi yanakuwa si ya muhimu au ya ghafla.Hivyo wakati unafanya mchakato wa kulipa madeni yako ni vyema kuepuka kukopa zaidi. Kuepukana na makosa haya ni muhimu kama una malengo ya kulipa madeni yako yote kwa muda mfupi.

 

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter