Home AJIRA Ishara 5 haupo tayari kuwa mjasiriamali

Ishara 5 haupo tayari kuwa mjasiriamali

0 comment 111 views

Licha ya picha nzuri tunazoziona katika mitandao ya kijamii kuhusu mafanikio wanayoyapata wajasiriamali, si kila mtu anafaa kuwa mjasiriamali. Ni kweli ujasiriamali unaweza kuleta maisha ya uhuru na faida kwa watu wanaojituma lakini ujasiriamali huo huo unaweza kuwa ni chaguo baya kwa watu wengine kwasababu si kila mtu anaweza kumudu vikwazo vinavyohusiana na ujasiriamali.

Kabla ya kuingia katika ujasiriamali ni muhimu kuwa na uhakika. Siku zote huwezi kuwa na uhakika kwa asilimia miamoja kuwa jambo unalotaka kufanya litafanikiwa kwa asilimia miamoja lakini hizi ni ishara tano zitakazokusaidia kujua kama uko/hauko tayari kufanya ujasiriamali na kufanikiwa:

Hauna msukumo binafsi

Si kila wakati katika ujasiriamali mambo yataenda sawa, hivyo kuwa na uwezo wa kujihamasisha na kujisukuma kufanya kazi peke yako bila kuambiwa na mtu katika kipindi ambacho unajisikia upweke, au mambo yakiwa hayako sawa kitakufanya ufanikiwe.

Lakini kama wewe ni mtu ambaye husubiria bosi wako akuambie nini cha kufanya na nini kinafuata basi hauko tayari kuwa mjasiriamali.

Hujaweka misingi

Kabla ya kuacha kazi unayolipwa kila mwezi kwaajili ya kuwa mjasiriamali ni vyema kujianzishia msingi. Msingi huo ni pamoja na mfuko wa dharula- kwasababu hakuna anaejua kesho itakuwaje na mambo yanaweza yasiende kama ilivyopangwa. Hivyo kama una fedha za kutosha kulipia bili zako, unaweza kumudu madeni yako, na una msingi wa kifedha unaoeleweka basi uko tayari kuwa mjasiriamali na hata kama mambo hayatokwenda kama ilivyopangwa itakuwa rahisi kwako kutafuta njia mbadala za kufanya mambo hayo hayaathiri ujasiriamali wako na maisha yako ya kila siku.

Huwezi kumudu kipindi kigumu

Biashara wakati mwingine inaweza kuwa katika wakati  mgumu inayoweza kukuchanganya, hali itakayo kulazimu kuendesha biashara yako  huku ukikumbana na mashinikizo kutoka katika kila upande.

Kama huna ujasiri wa kufanya maamuzi sahihi katika kipindi kigumu ni vyema kufikiria tena kuhusu ujasiriamali.

Hujafanya utafiti wa kutosha

Biashara yoyote ambayo unataka kuanza itahitaji utafiti. Kabla ya kuchukua hatua za kwanza unapaswa kuwa na ujuzi kuhusu nini cha kufanya ili kuwa na faida. Mtandao ya kijamii hutoa fursa ya kufanya utafiti mzuri utakaopelekea kujenga biashara yenye faida. Hivyo tumia fursa hiyo kujifunza kabla ya kufanya maamuzi.

Hauna shauku na biashara unayotaka kuanzisha

Shauku pekee haiwezi kujenga biashara lakini ni muhimu katika biashara. Kuna kipindi unaweza kuona kama biashara yako ni kazi , shauku yako itakukumbusha kila ulichonacho na itakusaidia kusonga mbele. Ikiwa hauna shauku ya biashara unayotaka kuanzisha basi hauko tayari kuwa mjasiriamali.

Hivyo chukua muda, kufanya utafiti, kutafakari na  kasha kuwa mkweli katika nafsi yako. Kufanya maamuzi yasiyo sahihi kunaweza kupelekea ukose vyote ikiwa ni pamoja na kazi yako uliyoajiriwa, muda wako, na fedha zako katika kitu ambacho ulikuwa unajua tokea mwanzo kuwa huna uwezo wa kukifanya na kikafanikiwa.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter