Home AJIRA Mamia walamba ajira ujenzi miundombinu Dodoma

Mamia walamba ajira ujenzi miundombinu Dodoma

0 comment 154 views

Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Godwin Kunambi amesema ujenzi wa miundombinu unaoendelea jijini humo umetoa ajira kwa watu wasiopungua 580, kati yao asilimia 70 ni wanaume na wanawake asilimia 30. Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa jiji hilo linafanya kila jitihada kuhakikisha ujenzi wa miundombinu ya barabara, stendi ya mabasi na soko la kisasa inakamilika huku wakitarajia kutumia Sh Bilioni 52 ambayo ni sawa na makusanyo ya ndani ya Sh. Bilioni 68 ambazo zilitengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/19.

Kunambi ameeleza kuwa miradi hiyo iliyoanza Desemba 2018 inategemea kukamilika Septemba 30 mwaka huu na hadi sasa Halmashauri imeshakusanya mapato ya Sh. Bilioni 48 ambayo ni zaidi ya asilimia 73 ya mapato ya ndani.

“Mkakati wa Halmashauri ya Jiji ni kuhakikisha kwamba ifikapo Juni 30 mwaka huu itavuka asilimia 100 ya kukusanya mapato yake”. Amesema Mkurugenzi huyo.

Vilevile ameongeza kuwa kutokana na kupungua kwa utegemezi wa viwanja katika jiji hilo, wana mpango wa  kufanya uwekezaji mkubwa ili kuzidi kuimarisha sekta ya miundombinu katika mji huo wa serikali. Aidha, ameeleza kuwa jiji hilo linafanya mazungumzo na mkandarasi mshauri ili kujua kuhusu uwekezaji ambao wameufanya na wanatarajia kufanya.

“Tumetafuta mkandarasi mshauri ambaye kabla ya Mei Mwaka huu, atawaambia namna ya kuendesha miradi hiyo mara itakapokamilika”. Amesema Kunambi.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter