Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo amesema waajiri ambao ni raia wa kigeni hususani wawekezaji katika sekta ya viwanda wanatakiwa kuzingatia Sheria za nchi hasa zile zinazohusu viwango vya mishahara. Ndikilo amesema waajiri hao wamekuwa na tabia ya kulipa wafanyakazi mishahara midogo isiyoendana na hali halisi ili hali serikali imeweka viwango vya mishahara nchini.
“Pamoja na kutoa ajira lazima wazingatie staha na si kuwadhalilisha wafanyakazi kwa kuwanyima haki zao stahiki zikiwemo za vifaa, likizo na fedha za likizo serikali haitokubali kuona wafanyakazi wananyanyaswa”. Amesema RC Ndikilo.
Kuhusu suala la vyama vya wafanyakazi, Mkuu huyo wa mkoa amesisitiza kuwa vyama hivyo vipo kisheria na kuwataka waajiri kutoa ruhusa kwa wafanyakazi wao kujiunga na vyama hivyo ambavyo vimelenga kufanya mawasiliano kati ya mwajiri na mwajiriwa.
“Sitapenda kusikia wafanyakazi wamefukuzwa kazi kwa kujiunga na vyama vya wafanyakazi kama jambo hili litaendelea sitakubali na wafanyakazi wawe huru kujiunga na vyama vya wafanyakazi kwani ni haki yao ya msingi na vipo kisheria vimeundwa kisheria, ikiwa ni jukwaa la kujadili na mwajiri watoe ushirikiano wa dhati ili kujenga mshikamano ambapo utendaji na uwajibikaji utakuwa mkubwa”. Amesema.