Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imepata kibali cha ajira za walimu wa Shule ya Msingi na Sekondari 6,949 na kada mbalimbali za afya 2,726 watakaoajiriwa chini ya Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini.
Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu, amesema ajira hizo zitajaza nafasi zilizoachwa wazi na watumishi waliokoma utumishi kutokana na sababu mbalimbali.
“Serikali imetoa kibali, maana mara baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kueleza kwamba atatoa ajira 6000 kwa walimu tulikuwa tunapata msukumo mkubwa kutoka kwa wananchi wakihoji kwanini TAMISEMI hatutangazi, taratibu za serikali lazima tupate kibali Menejimenti ya Utumishi wa umma” amesema Waziri Ummy
Waziri Ummy amesema kwa Shule ya Msingi wanatakiwa Walimu wenye daraja la IIIA wenye astashahada ya elimu ya msingi, elimu ya michezo, elimu ya awali na elimu maalum
Kwa upande wa mwalimu wa daraja la IIIB anatakiwa kuwa mhitimu wa stashahada ya ualimu wa elimu ya awali, msingi, elimu maalum huku mwalimu wa daraja la IIIC, anatakiwa kuwa mhitimu wa shahada ya ualimu masomo ya lugha ya historia, kiingereza, na jiografia.
Maombi ya ajira hizo yataombwa kwa njia ya mtandao kuanzia Mei 9 hadi 23, 2021, kupitia kiunganishi cha ajira.tamisemi.go.tz.