Vijana wa Tanzania waliosoma kuanzia elimu ya darasa la saba na kuendelea wametakiwa kujisajili kwenye ofisi za Kitengo cha Huduma za Ajira Tanzania (TaESA) kwa ajili ya kutafutiwa ajira nje ya nchi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhandisi Cyprian Luhemeja ametoa wito huo jijini Dar es Salaam alipofungua Kongamano la Ngazi ya Juu kuhusu Uhamiaji wenye Tija Barani Afrika.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mhandisi Luhemeja amesema kongamano hilo limelenga kupunguza changamoto za ajira, kuinua kiwango cha uwezo wa vijana na kuwajengea uwezo vijana kwenye mapambano ya kupata fursa za ajira.
Amebainisha kuwa Tanzania imesaini mikataba na mataifa mbalimbali kwa ajili ya kupeleka vijana kufanya kazi kwenye mataifa hayo katika kada mbalimbali kama vile Sheria, Uhasibu, Uhandisi, Udaktari na mafundi mbalimbali, huku akiwataka vijana kukubali kuungana na kufanya kazi kwa pamoja.
Amesema tafiti zilizopo zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwaka 2050, Bara la Afrika litakuwa na watu bilioni moja na milioni mia tano wenye nguvu ya kufanya kazi ambapo kwa sasa ni watu milioni mia saba tuu wenye uwezo wa kufanya kazi Barani Afrika.