Katika jitihada za kufanikisha azma ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ni vizuri kama elimu ya ufundi stadi ikapewa thamani na umuhimu kubwa. Mara nyingi hapa nchini, ufundi stadi umeonekana kama suluhisho la mwisho kwa vijana ambao wamekata tamaa na maisha. Vyuo vinavyotoa elimu hii vimekuwa havipewi kipaumbele katika jamii. Lakini ukweli ni kwamba, taasisi kama hizi zinatoa mchango mkubwa sana katika maendeleo ya taifa.
Unaweza kujiuliza kwanini wananchi wengi huona aina hii ya elimu kama kimbilio lao baada ya jitihada nyingine zote kufeli. Kwanini watanzania hawavipi heshima vyuo au taasisi kama hizi? Na je, ni nini taasisi kama hizi zinafanya ili kubadilisha mitazamo hii jamii iliyonayo? Serikali nayo inatoa msaada gani kwa sekta hii ili kuiboresha kama ilivyo kwa hizo nyingine?
Ukweli ni kwamba taasisi za ufundi stadi zimekuwa na mchango mkubwa sana katika kubadilisha maisha ya watu na kuleta maendeleo hapa nchini. Mfano hai wa hili ni Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi Tanzania (VETA). Mamlaka hii imebadilisha maisha ya mamia ya watanzania hasa vijana kutokana na mafunzo yake.
VETA imesaidia vijana wengi katika jamii kuweza kujiajiri na kujiingizia kipato. Wengi hasa wale ambao hawakupata nafasi ya kuendelea na masomo yao wamekuwa wakijiunga na mamlaka hii iliyo na matawi mengi kote nchini ili kujiendeleza kielimu pamoja na kiuchumi badala ya kukaa tu mitaani bila shughuli yoyote.
Kupitia ufundi stadi pia, vijana wengi wamefanikiwa kujifunza na kujikita katika ujasiriamali ili kujikwamua na umaskini. Mfumo huu wa elimu umekuwa kama tumaini jipya kwa wengi ambao ndoto zao za kujiunga na elimu ya juu hazikutimia. Vijana hawa wamepata fursa nyingine ya kutimiza ndoto zao na kubadili maisha yao kiuchumi. Vijana hawa pia kwa kujiajiri, nao wamefungua milango ya ajira kwa watanzania wengine na hivyo wamesaidia kupunguza tatizo la ajira hapa nchini.
VETA imekuwa na lengo la kuwawezesha watanzania kushiriki kiutendaji katika sera ya uchumi wa viwanda kupitia mafunzo mbalimbali wanayotoa. Mamlaka hii imewapa fursa vijana wengi hapa nchini na imekuwa ikiendelea kufanya hivyo.
Serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo kutoka sekta binafsi wanatakiwa kupaza sauti zao na kusaidia mamlaka kama hizi katika shughuli zao za kuwafikia watanzania wengi zaidi. Jamii ikipata mtazamo mzuri wa mamlaka hizi bila shaka vijana wengi zaidi watajiunga nazo na hivyo kuchangia moja kwa moja katika maendeleo ya taifa letu.