Kama umemaliza elimu yako na kuingia rasmi mtaani kuna fursa mbalimbali ambazo unaweza kutumia kujifunza na kupata ujuzi unaotakiwa katika ajira. Mara nyingi wahitimu wengi hukatishwa tamaa na ugumu wa soko la ajira na kujikuta wakishindwa kuendeleza elimu waliyopatiwa chuoni kwani wanakosa mahali pa kuanzia ili kuweza kuonekana na hatimaye kuajiriwa.
Endapo wewe ni mmoja kati ya wanaokumbwa na changamoto hii unaweza kufanya haya na kujiweka katika nafasi nzuri zaidi:
Anza kutumia LinkedIn – Kama bado hujajiunga na mtandao huu ni muda muafaka wa kufanya hivyo. Wakati watu wengi wakitumia muda mwingi katika mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Instagram na Snapchat, mtandao wa LinkedIn ni sehemu muafaka kwa masuala ya ajira ya biashara. Mara baada ya kufungua akaunti yako, unaweza kujiunga na makundi mbalimbali ili kupata taarifa muhimu ambazo zinaweza kukusaidia siku za mbele. Tengeneza mahusiano na watu kutoka sekta mbalimbali katika ulimwengu wa biashara.
Fanya kazi za kujitolea – Badala ya kutumia muda mwingi kuhanganika kutafuta kazi moja kwa moja, tumia muda huu kutafuta sehemu ambayo unaweza kufanya kazi kwa kujitolea bila kupata malipo yoyote. Hili ni jambo la msingi kwa wahitimu kwani ujuzi unaopata mahali hapo unaweza kuwa na mchango mkubwa katika ajira yako na unakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuajiriwa kuliko wale ambao hawajafanya kazi kabisa.
Tumia vizuri mitandao ya kijamii – Tofauti na matumizi yako wakati upo shule au chuo, wakati unajaribu kutafuta kazi ni muhimu kuangalia unachofanya katika mitandao ya kijamii. Mitandao ya kijamii ni utambulisho wa maisha yako hivyo unatakiwa kuonyesha yale ambayo yanakutambulisha vizuri kwa jamii kwani waajiri nao hutumia mitandao hii kujenga mahusiano na watu mbalimbali hivyo hakikisha inakutambulisha vizuri.
Wasiliana na unaotaka kufanya nao kazi – Andaa orodha ya watu, makampuni au biashara ambazo ungependa kufanya nazo kazi kisha tafuta mbinu za kuwasiliana nao huku ukieleza elimu yako na ujuzi ulionao. Makampuni mengi siku hizi huwa na tovuti, barua pepe na namba za simu hivyo unaweza kuwasiliana nao kirahisi na kueleza nia yako. Usikate tamaa pale wanapokataa na badala yake endelea kuwasiliana nao, jieleze kwa ufasaha na waonyeshe nini hasa unaweza kufanya.
Kwa kufuata hayo unakuwa katika nafasi nzuri zaidi kupata ajira na kufanikiwa.