Mara nyingi ili biashara iendelee zaidi huwa kunahitajika kiasi cha fedha ili kuleta mabadiliko hayo. Inawezekana mtiririko wa fedha ukawa si tatizo lakini ili kukuza biashara kiasi kikubwa cha fedha huhitajika hivyo hupelekea mmiliki kuchukua mkopo. Si vibaya kuchukua mkopo kwa ajili ya biashara yako ili hali lengo kubwa ni kuiboresha hivyo ikiwa unaenda kuchukua mkopo ni vyema ukifahamu mambo yafuatayo kuhusu viwango vya riba hususani katika benki za biashara.
Baadhi ya mikopo ya benki huhitaji malipo kufanyika mapema. Sawa mikopo ya muda mrefu inaweza kufika hadi miaka 30, lakini baadhi ya wakopeshaji huhitaji malipo ya mikopo mapema zaidi inaweza kuwa baada ya miaka kumi, mitano au hata baada ya mwaka mmoja. Hivyo ni muhimu kujua unaweza kulipa mkopo mzima baada ya muda gani na benki ipi inatoa huduma hiyo.
Viwango vya riba hupanda juu kadiri thamani ya mkopo inavyoongezeka. Kawaida mtu akikopa mkopo mkubwa basi ni dhahiri kuwa riba nayo itakuwa kubwa kutokana na thamani ya mkopo hivyo ni muhimu kujua hili kabla ya kuamua kiasi unachotaka kukopa.
Si vibaya kumuhusisha mke/mume/mshirika ikiwa unataka kukopa. Kama watu hawa wanamiliki asilimia katika biashara ni muhimu kuwahusisha kwasababu baadhi ya benki huhitaji dhamana za mali kama nyumba, gari, nk hivyo ni muhimu kuwa na makubaliano na mshirika mwenzako kuhusiana na maamuzi hayo ya kuchukua mkopo ili kila mmoja awe na uelewa hivyo itapelekea umoja zaidi ili kuhakikisha mkopo unalipwa na maendeleo yanafanyika.
Kwa kupata kiwango bora hatari nayo inakuwa ndogo. Hatari ya kukupa mkopo ikiwa ndogo hata viwango vya riba huwa katika hali nzuri. Hivyo jitahidi kuwa na mpango kuhusu kukua kwa biashara yako, fanya utafiti madhubuti kuhusu masoko, au unaweza kuingia ubia na kampuni kubwa ili kuhakikisha kuwa benki inakupa mkopo katika viwango vya riba rafiki.
Sawa, benki kubwa zinaweza kutoa kiwango bora cha riba lakini benki ndogo na za jamii huruhusu majadiliano kuhusu viwango na jinsi ya kupunguza zaidi pia huwa kuna uwezekano wa kufanya upanuzi wa mkopo wako wa biashara hivyo maamuzi ni yako kuhusu wapi utaona kuna uafadhali wa kuchukua mkopo kwaajili ya biashara yako.
Jambo la msingi ni kuwa na uhusiano wenye nguvu na benki yako. Hivyo jitahidi kujenga uhusiano mzuri na benki yako ili kwanza kujuana. Kwa benki kuwa na mahusiano na wewe na biashara yako hurahisisha majadiliano kuhusu mikopo na mambo mengine ambayo yanaweza kuinufaisha biashara yako.