Home BIASHARA Bidhaa za Tanzania zatamba soko la EAC

Bidhaa za Tanzania zatamba soko la EAC

0 comment 123 views

Mamlaka ya Maendeleo na Biashara Tanzania (TanTrade) imetaja bidhaa zinazohitajika kwa wingi kwenye soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), lengo likiwa ni kuwahamasisha wafanyabiashara kufanya biashara nje ya nchi na kuongeza pato la taifa. Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Biashara TanTrade, Twilumba Mlelwa amebainisha hayo.

Mlelwa ameeleza kuwa hadi sasa Tanzania imefanya mauzo ya wastani wa Shilingi bilioni 814.86 kupitia EAC. Amefafanua kuwa wafanyabiashara wanafanya mauzo Kenya ya wastani wa Sh. bilioni 536.90, Rwanda wastani wa Sh. bilioni 113.35, na Uganda wastani wa Sh. bilioni 90.19.

Pamoja na hayo, ameeleza kuwa kwa mwaka, fursa za biashara EAC ni asilimia 51 Kenya, asilimia 26 Tanzania, asilimia 17 Uganda, Rwanda asilimia 2 na Sudan Kusini asilimia 2 huku akitaja bidhaa ambazo zinauzwa kwa wingi kwenye soko hilo kuwa ni mbegu za pamba, mashudu ya pamba, alizeti, chikichi, mihogo na nafaka ambazo ni mahindi na pumba yake, maharage, mchele, ngano, kakao na chai, madini, saruji, vyombo vya plastiki, samaki na dagaa, vifaa vya ujenzi vya plastiki na vilainishi, vifaa vya umeme, vyandarua, vitenge, vikoi na nguo mbalimbali, vinywaji, mbolea za chumvi, chumvi, mafuta ya kupikia samaki na vifungashio.

“Jitihada za serikali ya Tanzania ni kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na nchi hizi ili kukuza uwekezaji na biashara. Uchambuzi wa kibiashara kwa mujibu wa Takwimu ya Kituo cha Biashara la Kimataifa (ITC) unaonyesha kuwa Tanzania ina fursa kubwa ya kuuza bidhaa mbalimbali katika nchi hizo”. Amesema Mlelwa.

Aidha amezitaka sekta binafsi kuwekeza kwenye soko la alizeti ili kuongeza uzalishaji wa mashudu ambayo yana soko kubwa Kenya, Uganda na Afrika Kusini.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter