Kufuatia agizo alilotoa Rais Magufuli hivi karibuni la kufungua soko la madini mkoani Mbeya, masoko mawili yamefunguliwa katika wilaya za Chunya na Mbeya mkoani humo. Akizungumza wakati wa ufunguzi wa soko kuu la madini, Mkuu wa huo, Albert Chalamila ametoa shukurani zake kwa Wizara ya Madini pamoja na Tume ya Madini kwa ushirikiano wao katika kukamilisha ufunguzi wa masoko hayo.
“Kama mnakumbuka Rais Magufuli alitupa siku saba kuhakikisha tunafungua soko la dhahabu Chunya, lakini pamoja na agizo hilo, ni utekelezaji wa Sheria za madini ili biashara ya uuzwaji na ununuzi wa madini yetu uwe wa wazi”. Ameeleza Chalamila.
Aidha ameongeza kuwa, kufuatia uzinduzi wa soko la Chunya uliofanyika tarehe mbili mei mwaka huu, tayari dhahabu ya gramu 2,000 imeshauzwa kwa Sh. Milioni 174.9 huku serikali ikipata milioni 12.4 na kueleza kuwa kupitia masoko hayo serikali, wachimbaji pamoja na wanunuzi watanufaika kwani biashara hiyo inafanywa kwa uwazi.
Naye Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara wa Tume ya Madini, Dk. Venance Mwasse, ameipongeza serikali ya mkoa huo kwa kutimiza agizo la kufungua masoko hayo. Dk. Mwasse ametaja masoko mengine ambayo yameshafunguliwa kuwa ni Geita, Singida, Kahama, Arusha-Namanga, Ruvuma, Shinyanga, Katavi, Dodoma, Tabora, Kigoma na Mara.