Mishumaa inaendelea kupendwa na watu wengi zaidi siku hadi siku. Ukiachana na kwamba mishumaa hutumika kama njia mbadala pale umeme ukikatika na vilevile kwenye shughuli mbalimbali, siku hizi watu wamekuwa wakitumia mishumaa kama mapambo nyumbani.
Unaweza kutengeneza mishumaa ya kila aina na kufanya biashara itakayokuingizia kipato kwa gharama ndogo. Hii inaweza kufanyika nyumbani au unaweza kununua mashine maalum kwa ajili ya kutengeneza mishumaa ya kila aina.
Mahitaji:
- Mafuta ya taa waxi/Nta (Paraffin wax)
- Asidi boriki na Stearine
- Rangi (ukipenda)
- Pafyumu (ukipenda)
- Utambi/uzi
- Umbo (mould) ya mshumaa (Zinapatikana katika mitindo na ukubwa tofauti)
- Jiko la mafuta ya taa/mkaa na sufuria na vijiko vya chakula
- Vifungashio vyenye lebo (Sio lazima ununue unaweza kubuni lebo inayokupendeza ili mradi mteja apate maelekezo)
Jinsi ya kutengeneza
Andaa maumbo ya mshumaa unayopendelea, weka utambi katikati ya chombo kwa kushikiza na ute wa mshumaa na funga utambi kwa juu. Weka sufuria jikoni kisha changanya nta kwa mfano kilo 1 kisha weka stearine vijiko 4 kutokana na kipimo hicho wakati unayeyusha nta unashauriwa kutumia sufuria mbili ambapo sufuria ya nje huwekwa maji kiasi na sufuria ya ndani huwekwa nta hiyo ili iweze kuyeyuka wakati unachemsha nta unaweza kuchanganya rangi, pafyumu, asidi na koroga hadi mchanganyiko uyeyuke, kisha epua, halafu mimina mchanganyiko kwenye maumbo na weka kwenye kivuli hadi mchanganyiko unaganda.
Ili kupata matokeo mazuri unashauriwa kusubiri hadi siku nyingine kisha ndio uondoe mishumaa taratibu kutoka kwenye maumbo, tayari kwa matumizi au kuuza.
Biashara hii kwa ujumla inalipa kwa sababu utengenezaji wake hauhitaji fedha nyingi hususani kama mtengenezaji ni mbunifu. Unaweza kuingiza fedha zaidi kama ukitengeneza mishumaa inayonukia kwani watu wanapendelea zaidi mishumaa ya aina hiyo pamoya na ile inayodumu kwa muda mrefu.
Jambo lingine la kuzingatia ni watu unaotegemea kuwauzia, kama mishumaa ya kawaida inauza zaidi ya ile inayonukia basi tengeneza bidhaa zako kulingana na mwenendo wa soko ili kuepuka hasara.
Soko
Kupata soko ni rahisi sana, kwanza unaweza kuanza kuwauzia watu wako wa karibu, pia unaweza kuwaambia watu wako wa karibu wawaeleze watu wao wa karibu, na unaweza kutumia mitandao ya kijamii kutangaza biashara yako ili kujipatia wateja zaidi. Jambo la kuzingatia kwa makini ni muonekano wa mishumaa yako. Mishumaa inayovutia itamhamasisha mteja kununua hata kwa matumizi ya mapambo tu.
Mfano wa kutengeneza mishumaa kwa video: https://www.youtube.com/watch?v=mmksNT5JuzQ