Intaneti imeendelea kurahisisha shughuli za biashara na ujasiriamali duniani. Kila siku fursa mbalimbali zinajitokeza mitandaoni hali ambayo imekuwa ikiwasaidia watu mbalimbali hususani vijana kujiajiri na kuweza kujikwamua kimaisha. Affiliate marketing (Uuzaji wa Ushirika) , ni moja ya njia rahisi ambazo watu wanaweza kutengeneza fedha kupitia mtandao.
‘Affiliate Marketing’ ni nini?
Ni ushirikiano wa kibiashara baina ya wafanyabiashara na wamiliki wa tovuti, blogu, mitandao ya kijamii nk, ambapo Affiliate (mmiliki wa tovuti au mitandao mingine iliyopo katika intaneti) hulipwa kamisheni katika mfumo wa asilimia na mfanyabiashara kulingana na makubaliano kila wakati mtu akinunua bidhaa husika kupitia linki yake (affiliate link).
Hivyo ili kuweza kufanya kazi hii Affiliate/mshirika/dalali anatakiwa kuwa na akaunti yenye wafuatiliaji (followers) wa nyaraka au habari ambazo huchapishwa (posts) mara kwa mara katika akaunti hiyo. Kuhusu mtandaoni inashauriwa kutengeneza tovuti au blogu kwani hii ni rahisi zaidi kufanya matangazo na hata kuandika zaidi kuhusu bidhaa hizo, pia watu wengine wanafanya biashara hii katika mitandao ya kijamii kama instagram, twitter nk. Hivyo kulingana na idadi ya watu ulio nao katika akaunti yako unaweza kutumia mtandao unaokufaa na utakaoweza kuwafikia wateja wengi zaidi.
Faida za kufanya Affiliate marketing:
- Hakuna gharama za kutengeneza bidhaa, kununua wala kuhifadhi bidhaa husika. mtu yeyote anayefanya kazi hii anakuwa hana jukumu la kufanya mambo hayo matatu. Kazi yake pekee ni kuhakikisha kuwa wateja husika wa bidhaa hiyo wanatembelea tovuti au akaunti ya mtandaoni ya biashara husika na kuweza kufanya manunuzi au hata kujisajili kulingana na makubaliano.
- Mtu yeyote anaweza kufanya kazi hii hata kama hana ujuzi wa masuala ya teknolojia (IT) na fedha. Mtu yeyote anayetaka kufanya kazi hii anatakiwa kujua kuwa hakuna gharama zozote ambazo atatumia kujiunga/kujisajili hivyo hakuna hatari ya kupata hasara. Jambo la msingi ni kutafuta programu ya masuala haya- iwe inakubali katika nchi za Afrika kwasababu si kila programu inafanya kazi dunia nzima, kisha jisajili na kuanza kazi.
- Wauzaji hupata nafasi ya kuuza bidhaa zaidi kwa wateja wengi kutoka sehemu mbalimbali bila kutumia muda mrefu kuwatafuta wateja hao. Pia ni rahisi kwa wauzaji kujua bidhaa zinazouzika katika wakati husika.
- Ni rahisi kufanya kazi hii muda wowote. Hivyo ikiwa mtu ameajiriwa anaweza kufanya kazi hii muda ambao anakuwa hayupo kazini ili kuweza kuongeza kipato zaidi.
Hasara za kazi hii:
- Si rahisi kutengeneza na kuitangaza brandi binafsi, kwasababu kazi yako ni kutangaza brandi za watu wengine.
- Ikiwa mfanyabiashara anapata wateja wachache kutoka kwako, hata kamisheni yako inakuwa ndogo. Hivyo juhudi zako katika kazi hii zinaweza kukuletea faida au kusababisha usiingize fedha kabisa.
- Mfanyabiashara huamua kiasi cha kukulipa na muda gani. Hiyo inaweza kuleta changamoto ikiwa unahitaji fedha za dharula/haraka.
- Wakati mwingine matangazo ya biashara yanaweza yasiendane na bidhaa hizo katika hali ya uhalisia. Hii inaweza kufanya watu wanaokufuatilia mtandaoni wasiamini machapisho yako na wengine kufikia hatua ya kuacha kukufuatilia.
Mbali na hasara hizo, kazi hii inawasaidia watu mbalimbali duniani kupata kipato na hata wengine wamefanikiwa kupitia kazi hii. Jambo la msingi ni kufanya utafiti wa kina kuhusu programu ya kujiunga, na biashara unayotaka kuitafutia masoko ili mchakato mzima uende sawa. Pia ni muhimu kuwa makini mitandaoni ili kuweza kujiepusha na masuala ya utapeli.
Moja ya programu inayotumika na wengi kufanya kazi hii ni programu iitwayo JVZoo https://www.jvzoo.com/ bonyeza linki hii kuona inavyofanya kazi.