Mitandao ya kijamii imeendelea kuwa na mchango mkubwa katika sekta ya biashara. Wafanyabiashara wengi wamekuwa wakitumia mitandao ya Facebook na Instagram kujitangaza na kuwafikia wateja kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa urahisi na gharama nafuu kabisa. Lakini ili kupata mafanikio haya unajua unahitaji kufanya nini katika mitandao yako?
Hapo chini ni baadhi ya vitu ambavyo unatakiwa kufanya kama mfanyabiashara au mjasiriamali mtandaoni ili kuhakikisha wateja wanakupata kirahisi.
Weka taarifa zote muhimu: Kama lengo ni kupata wateja, unatakiwa kuweka wazi taarifa zote za msingi ili pale mteja anapotembelea ukurasa wako, apate taarifa zote za msingi mara moja. Taarifa kama mahali uliopo, huduma unazotoa, namba ya simu na eneo ulipo ni muhimu kwani zina nafasi kubwa katika maamuzi ya mteja. Hakikisha ukurasa wako wa biashara haukosi taarifa zote za msingi.
Hakikisha taarifa zako zinafanana: Pamoja na kuweka taarifa zako zote, unatakiwa kuhakikisha kuwa taarifa zote zipo sawa ikiwa unatumia mitandao mbalimbali ya kijamii. Kuwa na taarifa tofauti humuweka mteja kwenye wakati mgumu na hata kupelekea kukosa wateja kabisa. Ni muhimu kupitia taarifa zako zote na kuhakikisha kuwa hazitofautiani. Usiwachanganye wateja wako!
Weka Picha na video nzuri: Ikiwa wewe ni mtu ambaye asilimia kubwa ya biashara yako inafanyika mtandaoni, ni muhimu kuwekeza katika kupata picha na video nzuri kwa kuwa hii itafanya ukurasa wako uvutie watu wengi zaidi kutembelea. Hakuna mtu ambaye atavutiwa kununua kutoka kwako ikiwa havutiwi na kile anachokiona kwenye picha. Wekeza kwenye picha nzuri ili kuwavuta watu wengi zaidi kutembelea.
Jibu maoni/ujumbe: Hili lipo wazi japokuwa ukweli ni kwamba, wafanyabiashara wengi hawajibu maoni wanayotumia kwenye mitandao ya kijamii. Usipitie tu maoni hayo, yajibu ipasavyo. Wasiliana na wateja wako. Angalia ujumbe/maoni/ushauri/swali unalotumiwa na chukua muda kujibu. Tenga muda maalum kwenye mitandao kwa ajili ya kuzungumza na wateja wako. Ikiwa hujibu maoni wala ujumbe mfupi, unakosa fursa na kutengeneza mahusiano mazuri hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kukosa wateja.
Fahamu muda gani ni mzuri: Fanya utafiti kujua ni muda gani asilimia kubwa ya wateja wako wapo hewani kwani huo ndio muda mzuri kwako kutumia mitandao na kuwafikia moja kwa moja. Kwa kufanya hivyo unakuwa na uhakika kuwa ujumbe unawafikia na wanaona bidhaa au huduma yako.
Ukurasa usiwe biashara tu: Hii ni moja kati ya vitu ambavyo ni kero kubwa kwa wateja mtandaoni. Hata kama unatafuta wateja ni muhimu kuhakikisha kuwa biashara haitawali ukurasa wako kwa asilimia 100. Siku nyingine unaweza kuweka picha yako, unaweza kuweka picha za wateja wakifurahia bidhaa yao n.k. Epuka ukurasa wako kuwa na mtiririko wa matangazo na biashara pekee kwani hii huwachosha watu na kuwafanya wasirudi tena katika ukurasa wako siku nyingine.
Wateja/Marafiki zako mtandaoni wanataka nini?: Kwa kufanya hivi, inakuwa rahisi kuwapa kile wanachotaka. Hii ni njia nzuri ya kuanzisha mazungumzo na kujenga mahusiano mazuri ya kudumu na wateja wako.