Kampuni ya Magnit ya nchini Urusi imeeleza nia ya kununua bidhaa mbalimbali kutoka Tanzania ikiwemo matunda.
Hayo yameelezwa katika mkutano ulioratibiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kati ya kampuni hiyo na kampuni za Tanzania.
Mwakilishi wa Kampuni hiyo ameeleza kuwa wanayo nia ya kununua bidhaa mbalimbali kutoka Tanzania ikiwemo ndizi, nanasi, embe, passion, papai na parachichi.
Bidhaa nyingine ni kahawa, korosho, alizeti, viazi na soya.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Biashara kutoka TanTrade Emmanuel Miselya amewaeleza washiriki kuwa mkutano huo umelenga kuendeleza na kuimarisha mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na Urusi.
Amewataka wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamkia fursa za masoko kwa bidhaa zinazohitajika na kampuni hiyo ili kukuza uchumi wa nchi na kuendelea kunufaika na mahusiano mazuri baina ya nchi hizo mbili.