Mfanyabiashara anapoanzisha biashara yake huwa na matumaini ya maendeleo lakini si kila mfanyabiashara huzingatia suala la utafiti wa kina kuhusu biashara anayotaka kuanzisha hali ambayo inapelekea biashara hiyo kushindwa kuendelea kwa sababu mfanyabiashara husika hakuzingatia yafuatayo:
Kuzalisha bidhaa au huduma iliyo chini ya kiwango
Mfanyabiashara anatakiwa kuelewa kuwa siku zote mteja hushabikia bidhaa au huduma yenye ubora wakuridhisha hivyo kama unatoa huduma au kuuza bidhaa zisizokuwa na kiwango basi tegemea mauzo ya chini au kukosa mauzo kabisa kwa kuwa wateja huenda sehemu yenye bidhaa au huduma nzuri.
Kuanzisha biashara wakati usio muafaka
Kwa mfano ni kipindi cha jua na wewe unawaza kuanzisha biashara ya makoti ya mvua, masweta na mitandio. Kawaida hapo huwezi kufika mbali sana na biashara hiyo kwa sababu watu hawahitaji bidhaa hizo kipindi cha jua hivyo kupelekea biashara kutoendelea.
Kutoona thamani ya mteja
Jambo la muhimu ambalo mfanyabiashara anapaswa kuzingatia ni mteja. Kama hakuna mteja basi hakuna biashara hivyo moja ya mambo ambayo yamewaharibia sifa wafanyabiashara wengi na kupelekea kufunga biashara zao ni lugha mbovu kwa wateja na kutokuwajali pale wakifika katika eneo la biashara.
Kutokupanga bei vizuri
Hii inaweza kupelekea mfanyabiashara kukosa wateja kwa sababu kama ukiweka bei kubwa basi wateja hawatokuja kukuungisha na ukiweka bei ndogo sana itakuwa vigumu kutekeleza shughuli zinazohusu biashara na binafsi kwani hutopata faida, jambo linaloweza kupelekea kufunga biashara. Unashauriwa kupanga bei ya kati ambayo haitokuumiza wewe na wakati huo itawavutia wateja wako.
Umuhimu wa bidhaa au huduma
Unaweza kuwa na washindani wengi lakini je, ni kitu gani ambacho wateja watakipata katika biashara yako ambacho hawawezi kukipata kwa washindani wako? Ukipata jibu la hili swali basi itakuwa rahisi kufanya maamuzi sahihi na yenye manufaa kwako na kwa jamii kwa ujumla.