Kama mojawapo ya harakati za kujiongeza na kutengeneza kipato, watu wengi zaidi wamekuwa wakijiajiri kupitia biashara ndogo ndogo. Japokuwa wengi wamekuwa wakiona mafanikio na kutoa ushuhuda kuwa biashara inalipa, wengine hawakupata bahati hiyo na kujikuta wakipata hasara na kuwa katika hali mbaya kiuchumi. Ni kweli kupitia sekta hii, wengine wameweza kujiajiri na hata kufikia hatua ya kuajiri wengine. Vilevile, serikali nayo inafaidika na biashara hizi kupitia ukusanyaji wa mapato. Hii inamaanisha kuwa, biashara ni nguzo moja muhimu katika kuleta maendeleo hapa nchini. Lakini swali la msingi hapa ni, unafahamu vizuri soko lako?
Ni vizuri kujiuliza swali hili kama unafikiria kufanya biashara. Hata wale ambao tayari ni wafanyabiashara lakini wanataka kufika mbali zaidi kupitia hicho wanachofanya. Msingi wa biashara yoyote ile ni soko kwani hakuna biashara ambayo itafanikiwa pasipo kupokelewa vizuri na watu. Hivyo swali hili linabeba uzito mkubwa na mfanyabiashara anapaswa kujipanga na kuhakikisha kuwa anafahamu anaowalenga mwanzoni kabisa mwa mipango yake. Kama mfanyabiashara unamuuzia nani? Unalenga kundi fulani maalum kuwa wateja wako wakubwa?
Ukitafakari hayo ni vizuri kuwa na mipangilio madhubuti ambayo itakusaidia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo uliyojiwekea. Mfano umedhamiria kufanya wanafunzi wa vyuo kuwa wateja wako, utafanyaje kuhakikisha bidhaa zako zinawafikia kwa urahisi? Utakabiliana vipi na ushindani? Utakuwa unauza kwa bei iliyo rafiki kwao?
Ili kuona biashara yako inafika mbali na kukuletea faida ni vizuri kama ukafahamu vizuri unawalenga wakina nani haswa. Kufahamu soko lako kunasaidia kujua ni namna gani ya kutangaza bidhaa zako, namna gani bidhaa zako zitawafikia watu wengi na vilevile vinampa wepesi mfanyabiashara kuwa makini na kuelewa nini wateja wake wanahitaji bila ya kuingia hasara tofauti na yule ambae hana soko maalum hivyo anatumia muda mrefu zaidi kujitangaza, kujenga uaminifu na kuwavutia wateja. Kufahamu ni aina gani ya watu huvutiwa na kununua bidhaa zako zaidi humsaidia mfanyabiashara kufahamu ni wapi haswa anatakiwa kuwekeza fedha zake ili uwekezaji wake umfaidishe baadae.
Baada ya kufahamu soko lako, biashara yako ina nafasi kubwa ya kukua kama utatumia mbinu bora zaidi kujitangaza ili kuwafikia watu wengi zaidi. Mfano kama unawalenga wanafunzi wa chuo, unaweza kujitangaza kwa kiasi kikubwa kupitia mitandao ya kijamii. Matumizi ya mitandao hii yamerahisisha biashara kwa kiasi kikubwa hivyo mfanyabiashara akitumia mitandao vizuri, anaweza kuwafikia watu wengi zaidi kwa kutumia gharama ndogo na muda mfupi.
Sekta hii ni muhimu katika maendeleo ya nchi yoyote na hivyo kuna ushindani mkubwa kuhakikisha kila mfanyabiashara anavutia wateja kuja kwake. Kuelewa soko inasaidia kwa kiasi kikubwa kukuweka katika nafasi nzuri kibiashara. Wafanyabiashara wanatakiwa kufanya utafiti ili kubaini wakina nani haswa ni soko lao na ni nini wanahitaji kutoka kwako.