RC Makalla ameongeza siku hizo ili kutoa muda wa kutosha kwa machinga hao kuhama ambapo amesema muda alioongeza ukimalizika asionekane mfanyabiashara yoyote kwenye maeneo yaliyokatazwa.
Akizungumza na wafanyabiashara Kariakoo, RC Makalla ameelekeza eneo la DDC liboreshwe ili liweze kupokea wafanyabiashara wengi zaidi tofauti na sasa ambapo linatumika kuuza vyakula na vinywaji.
Aidha RC Makalla amefurahishwa na mwitikio mzuri wa wafanyabiashara kuhamia kwenye maeneo yaliyotengwa na kutoa wito kwa wengine kutumia muda uliotolewa kuhama.
Hata hivyo RC Makalla ameyataja makundi ya wafanyabiashara wanaotakiwa kuhama ni pamoja na wanaofanya biashara kwenye maeneo ya watembea kwa miguu, hifadhi ya barabara, mbele ya Maduka, kwenye maeneo ya umma na waliojenga vibanda juu ya mitaro na mifereji.
Miongoni mwa sababu zinazofanya serikali kuamua kuwapanga vizuri machinga ni kupotea kwa mandhari ya Jiji kutokana na uchafu, ongezeko la ajali na foleni na sababu za kiusalama.
Nyingine ni upotevu wa mapato ya serikali kutokana na wafanyabiashara wakubwa kuwatumia machinga kukwepa kodi.