Zaidi ya magari 2,000 yanapokelewa kila siku kupitia Bandari ya Dar es Salaam ambapo asilimia 60 ya magari hayo huenda nchi jirani.
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kupitia Mkurugenzi wake Mrisho Mrisho amesema hayo mjini Bagamoyo.
Amesema idadi hiyo inatokana na maboresho katika Bandari ikiwa ni pamoja na maboresho katika eneo lenye ukubwa mita za mraba 76,000.
Mrisho amesema eneo hilo kwa sasa linauwezo wa kubeba magari zaidi ya 6,000 na limefungwa na miundombinu ya kisasa kuwezesha ulinzi na usalama.
Mkurugenzi wa Huduma za Usalama katika Mamlaka ya Bandari nchini amesema kuna zaidi ya kamera za ulinzi (CCTV) 450 ambazo zimefungwa katika bandari ya Dar es Salaam ili kuimarisha usimamizi wa bandari hiyo.
Mpanda amesema, Mamlaka pia imefunga midaki (Scanners) katika bandari hiyo ili kubaini mizigo ambayo imepakiwa kwenye makasha (containers). Akizungumza na wanahabari katika kikao kazi kinachoendelea Bagamoyo mkoani Pwani, Mpanda amesema Mamlaka pia inaendelea na mpango wa kuunganisha Bandari zote 86 katika mfumo wa kisasa utakaowezesha utambuzi wa shughuli zote katika bandari.
“Tumeweka mifumo hii ya kiteknolojia lakini pia kuna askari na doria ambazo zinafanyika ili kuhakikisha usalama na kudhibiti uhalifu bandarini,” amesema Mpanda.