Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameeleza kutofurahishwa na biashara za magendo zinazoendelea wilayani Kyerwa mkoani Kagera na kuwataka viongozi wa wilaya hiyo kujitathmini wenyewe. Majaliwa amemuagiza Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa mkoa huo, Adam Ntogha kumsimamisha kazi Afisa wa Forodha katika mpaka wa Mulongo Peter Mtei kwa tuhuma za kujishughulisha na biashara za magendo. Waziri Mkuu ametoa agizo hilo wakati akizungumza na viongozi wa mkoa huo katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya kikazi ya siku nne.
“Biashara za magendo zinafanyika bila ya wao kuchukua hatua, mnatia aibu yaani hakuna kazi inayofanyika. Viongozi wa wilaya ya Kyerwa mjipime wenyewe, mialo mingi katika wilaya yenu inatumika kwa biashara ya magendo na butura”. Amesema Waziri Majaliwa.
Mbali na hayo, Waziri Mkuu pia ameeleza kuwa, katika mwalo wa Mulongo ulipo kwenye eneo ambalo Tanzania inapakana na Uganda na Rwanda, biashara za magendo na butura zimekuwa zikifanyika huku viongozi wakiwa hawachukui hatua yoyote. Majaliwa pia amemuagiza Meneja wa TRA kutowasimamisha kazi watumishi wasio waadilifu kutoka kituo kimoja cha forodha na kuwapeleka kingine kwani wanaenda kuendeleza biashara za magendo na kuikosesha serikali mapato. Aidha, Waziri Mkuu amemuagiza Meneja huyo kufanya ukaguzi kwenye vituo vyote vya forodha mkoani humo, kuongeza idadi ya watumishi na kudhibiti vitendo vya rushwa.