Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amewaambia wafanyabiashara mkoani Tanga kuwa, serikali imeanza mchakato wa kulipa madai ya marejesho ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT Refund) kwa makampuni na wafanyabiashara mbalimbali ikiwa ni pamoja na waagizaji wa sukari za viwandani ambao madai yao yamehakikiwa kuanzia mwezi huu.
Hatua hiyo inafuatia maombi ya wafanyabiashara wa mkoa huo ambao walitaka serikali kuwalipa wanaodai kurudishiwa fedha zao zinazotokana na kufanya biashara zao nje ya nchi pamoja na wazabuni mbalimbali. Dk. Mpango ameeleza kuwa malipo hayo yamechelewa kunatokana na udanganyifu mkubwa unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara.
“Kuna baadhi ya wafanyabiashara sio waaminifu, mfano tulipofanya uhakiki tuligundua madai hewa ya pembejeo ya zaidi ya shilingi bilioni 87”. Amesisitiza Waziri huyo.
Vilevile, Dk. Mpango ametumia nafasi hiyo kuwahakikishia wafanyabiashara wote nchini kuwa serikali inatengeneza mazingira mazuri ili kumpa nafasi kila mwananchi mwenye nia njema kufanya biashara iliyohalalishwa na itakayomletea faida na kuwezesha serikali kukusanya kodi bila uonevu. Mbali na hayo, Waziri huyo pia ametoa wito kwa wafanyabishara kuendelea kuishauri serikali kuhusu mbinu bora za kukusanya kodi ili serikali iweze kufahamu na kuboresha maeneo yaliyo na upungufu.