Mkurugenzi wa Sensa ya Takwimu za Kijamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephraim Kwesigabo amesema Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Machi 2019 umeongezeka na kufikia asilimia 3.1 kutoka asilimia 3.0 kwa mwaka ulioishia Februari 2019.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa ya mfumuko wa bei jijini Dodoma, Kwesigabo ameeleza kuwa ongezeko hilo limetokana na bidhaa zisizo za vyakula kama mavazi na viatu (3.4%), kodi ya pango (4.7%), mafuta ya taa (8%), malazi hotelini (5.7%), chakula na vinywaji (4.6%), dizeli (8.3%), mkaa (13.1%), kuni (27.2%) pamoja na huduma za afya (1.8%).
Aidha, Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa Machi 2019 umepungua hadi asilimia 0.1 kutoka asilimia 0.5 kwa mwaka ulioishia Februari mwaka huu.
“Kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa taifa kumechangiwa hasa na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi cha mwaka ulioishia Machi mwaka huu ikilinganishwa na bei za Machi 2018”. Amefafanua Kwesigabo.
Akizungumzia hali ilivyo kwa upande wa Afrika Mashariki, Mkurugenzi huyo amesema mfumuko nchini Uganda umeendelea kuwa asilimia 3.0 kama ilivyokuwa mwaka ulioishia Februari mwaka huu.
“Kwa upande wa Kenya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Machi 2019 umeongezeka hadi asilimia 4.35 kutoka asilimia 4,14 kwa mwaka ulioishia mwezi Februari 2019”. Amesema Kwesigabo.