Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema anataka kurudisha hadhi ya Tanga iwe Tanga yenye viwanda, Bandari kubwa lakini pia Tanga ya uvuvi.
Rais Dkt. Samia amesema hayo wakati alipotembelea Bandari ya Tanga Machi 01, 2025.
Rais Samia amesema “kwa muda mrefu wana Tanga na Watanzania tulitamani kuona manufaa zaidi kwa Bahari zetu na kuona Meli kubwa zikitia nanga kwenye Bandari zetu ikiwemo Tanga na vijana wakipata ajira Bandarini, kusudio hilo kwa muda mrefu halikuwezekana kutokana na ukosefu wa miundombinu, ndio maaana Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) iliyopita waliliona hilo wakatutaka Serikali tuboreshe Bandari zetu.
Bandari ya Tanga mpaka sasa hivi imehudumia tani milioni 1.2 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya tani laki 7 ukilinganisha na mwaka 2019/2020 kwa kuongeza uwezo wake wa kuhudumia Meli kubwa zaidi na kuhudumia Meli mbili kwa wakati mmoja, haya ni maendeleo makubwa sana, maboresho haya yameongeza pia mapato ya Serikali, nataka kurudisha hadhi ya Tanga iwe Tanga yenye viwanda, yenye Bandari kubwa lakini pia Tanga ya uvuvi.”
“Kama alivyosema Waziri muda wa kushusha Meli Bandari ya Tanga sasa hivi ni siku mbili tu, na nilikuwa nam-challenge Mkurugenzi Mkuu wa Bandari kwamba Dar es salaam kwa ufanisi imepitwa na Bandari ya Tanga, Tanga ni siku mbili tu, Dar es salaam wanachukua muda mkubwa kidogo lakini ni kwasabababu ya msongamano pale baada ya kufanya maboresho ya bandari, maboresho ambayo kwa kiasi fulani yalini-cost kidogo yalinigharimu lakini baadaye Watu wameona faida yake.”
Amebainisha kuwa, Serikali imetekeleza maelekezo ya Ilani ya CCM ya kuboresha Bandari ya Tanga kwa kiwango kikubwa ambapo amesema Tanga kwa upande wa Bandari hakuna wanachoidai Serikali.
“Nafurahi kwamba tumetekeleza maelekezo hayo ya Chama kwa kuleta Tsh. bilioni 429 hapa Tanga kuimarisha Bandari, katika hilo Tanga haitudai, kwenye hili la Bandari Tanga hamtudai, mnatudai mengine lakini sio kwenye Bandari, ingawa bado tutaendelea kufanya maboresho ili ifikie ya kiwango tunachokitaka” ameeleza Rais Dkt Samia.