Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti amewataka watendaji kuhakikisha vitambulisho 35,000 vilivyotolewa kwa awamu ya pili vinawafikia walengwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu. Brigedia Gaguti amesema hayo kwenye hafla iliyowashirikisha wakuu wa wilaya saba za mkoa huo, wakurugenzi, wenyeviti wa halmashauri pamoja na Meya wa manispaa ya Bukoba.
Gaguti amezitaka mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha hadi takwimu za wafanyabiashara wote zinakusanywa ndani ya wiki mbili zijazo lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi anatambuliwa na kulipa tozo au kodi stahiki kwa mujibu wa kanuni na Sheria
Kwa upande wake, Meneja wa TRA mkoani humo Adam Ntoga amesema mfanyabiashara anayestahili kitambulisho kilichotolewa na Rais Magufuli ni Yule ambaye mauzo yake ya siku hayafiki Sh. 11,000.
“Hata kama mfanyabiashara ana mtaji wa Sh. 5,000, lakini anauza bidhaa zake kwa siku na kupata Sh. 11,000 au zaidi kwa siku huyo hastahili kupata kitambulisho, kinachoangaliwa hapa si mtaji wa mfanyabiashara alionao bali ni mauzo yake”. Ameeleza Ntoga.