Watu wengi wamekuwa na mtizamo kuwa bidhaa za ndani hazina ubora na viwango vya juu, jambo ambalo si kweli. Kwasababu taasisi zinazohusika na masuala ya ubora zimekuwa zikiwahamasisha wajasiriamali na wafanyabiashara nchini kutengeneza bidhaa zenye viwango vya juu na ubora wa kuridhisha ili kuweza kuteka soko la ndani na nje ya nchi. Hivyo kama umekuwa ukinunua bidhaa zinazotengenezwa nchini basi umesababisha mambo mazuri yafuatayo:
Ajira
Biashara haiwezi kuendelea kama hakuna wateja, na bila wateja mjasiriamali atashindwa kujiajiri na kufunga biashara yake. Lakini kama watu wa ndani wakitoa sapoti kwa kununua bidhaa za wajasiriamali wa ndani basi ni dhahili kuwa biashara itapata maendeleo, na kumfanya mjasiriamali aweze kutoa ajira hata kwa watu wengine hivyo kupunguza idadi ya watu wasio kuwa na ajira mtaani. Hivyo kama umekuwa ukinunua bidhaa za ndani kwa namna moja au nyingine umewasaidia watu mbalimbali kupata ajira na kujikimu kimaisha.
Maendeleo ya uchumi wa ndani
Kuna msemo unaosema “mabadiliko huanza na wewe” hivyo hata kwenye masuala ya uchumi wa ndani mabadiliko hayawezi kufanyika kama watu wa ndani wenyewe hawatoi sapoti katika bidhaa au huduma zinazotengenezwa nchini. Hivyo kama watu wanawasapoti wajasiriamali wa ndani ni rahisi kwa watu wa nje pia kuvutiwa na bidhaa au huduma za wajasiriamali hao hivyo kuleta mafanikio katika biashara zao na kukuza uchumi wao na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Huduma za kipekee
Ni dhahili kuwa wajasiriamali wa ndani hujali zaidi mteja akiridhika na bidhaa au huduma kuliko fedha. Wengi wao hutoa huduma za kipekee ili wateja waweze kuja tena na tena. Hivyo kama unafurahishwa na huduma nzuri, pendelea kununua bidhaa au huduma katika biashara ndogo ndogo za ndani ili uweze kujipatia huduma za kipekee, na kuridhika na bidhaa au huduma husika.
Vile vile wajasiriamali hupata ujasiri wa kupambana zaidi hasa pale wakiona watu wa ndani wananunua bidhaa zao. Hivyo basi tambua kuwa kupitia manunuzi yako ya bidhaa na huduma za wajasiriamali wa ndani unawasaidia watu kufikia malengo yao na kufanikiwa katika maisha. Si vibaya kununua bidhaa za nje lakini mwisho wa siku kuna umuhimu mkubwa sana wa kufurahia bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali/wafanyabiashara wa ndani hasa kama unajali maendeleo ya watu wengine na ya nchi.