Katibu wa Kikanda wa Taasisi ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Dodoma, Idd Senge amesema taasisi hiyo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wanatarajia kuanzisha mpango maalumu wa kutoa mashine za EFD kwa wafanyabiashara mkoani humo ili kuboresha ukusanyaji wa kodi.
Katibu huyo ameeleza kuwa mwanzoni programu hiyo maalum italenga kuwasaidia wafanyabiashara angalau 1,000 kwani maandalizi ya mpango huo yamefikia katika hatua endelevu. Ili kukamilisha programu hiyo, wanufaika watatakiwa kufungua akaunti katika benki ya NBC ambapo benki hiyo itakuwa ikifanya makato ya fedha baada ya kununua mashine hizo.
Pia amesema kuwa ili kuwapata wafanyabiashara wa kuwapa mashine hizo, TCCIA na TRA itatangaza wafanyabiashara wanaostahili kupata mashine hizo kwani imetambulika kuwa wafanyabiashara wengi wanaostahili kuwa na EFD jijini humo hawana uwezo wa kuzinunua.
Benki ya NBC imeweka masharti nafuu ili mkopo wa kununua mashine hizo uweze kurudishwa. Lengo la taasisi hizo kufanya makubaliano na NBC ni kuwaunga mkono wafanyabiashara ili kuwawezesha kupata mashine hizo.