Hafla mbalimbali za kukuza mtandao wa kibiashara zimekuwa zikiandaliwa ili kuwakutanisha wafanyabiashara na wateja. Hata katika zama za utandawazi na matumizi ya mitandao, hafla hizo bado zina umuhimu kujenga uhusiano wa ana kwa ana na mteja ili kuongeza mauzo.
Hivyo ikiwa umehudhuria hafla inayolenga kukuza mtandao wa biashara, kama mfanyabiashara unatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo:
- Ukifika katika hafla husika, epuka kukaa na watu unaowajua. Badala yake jitambulishe kwa mtu mwingine yoyote usiyemjua. Hii itakusaidia kukuweka katika hali sahihi kiakili na kujua kilichokupeleka katika hafla husika.
- Ukikutana na mtu yoyote kwa mara ya kwanza jitahidi kusikiliza zaidi ya kuuza bidhaa yako. Ni muhimu kutengeneza uhusiano na kumjua mtu huyo kabla ya kuelezea bidhaa yako.
- Weka mawasiliano yako kama simu na kadi zako za biashara katika mahali ambako ni rahisi kuzifikia, na si rahisi kuharibika.
- Wakati wa kumpa mtu kadi yako, andika maelezo ya ziada juu yake. Hii itasababisha mpokeaji kuhisi kuwa anapokea kitu maalum.
- Wakati wa kupokea kadi ya biashara kutoka kwa mtu, chukua muda wa kujiandikia noti juu ya kadi hiyo, kwa mfano mahali mlipokutana. Ikiwa unafanya hivi wakati unazungumza na mtu huyo, ili kumuonyesha kuwa una nia ya kuwasiliana naye zaidi.
- Wakati wa mazungumzo katika hafla ya mitandao, jitahidi kutumia majina ya kwanza ya kila mtu wakati wa mazungumzo kwasababu wwatu hufurahia zaidi wakiitwa majina yao ya mwanzo. Pia itakusaidia kuwakumbuka mazungumzo yakiisha.
- Badala ya kujielezea kwa mtu mpya, tumia muda mwingi kuuliza maswali. Utajifunza mambo mengi.
- Tikisa kichwa kuashiria kuwa unasikiliza kwa makini na kutilia maanani maneno anayosema mtu mwingine. Hii itampa nguvu mtu huyo kuendelea kukuelezea mambo mbalimbali.
- Wakati mtu anaongea na wewe hakikisha kuwa unamuangalia moja kwa moja. Kumpa mtu umakini kamili na macho yako kutawapa moyo kushiriki zaidi.
- Mahali pazuri kwa kupata mahusiano mapya ni karibu na chakula, karibu na sehemu za vinywaji na karibu na mlango. Watu wengi hupendelea kukaa maeneo hayo.
- Siku zote epuka kumfuata mtu akiwa anaongea na simu. Subiri amalize kisha mfuate kwa ajili ya mazungumzo.
- Baada ya mtu huyo kushiriki kitu na wewe, waulize swali lingine juu ya kile walichosema. Hii inaonyesha kuwa unasikiliza na unajali kile wanachokuambia.
- Ili kuonyesha ustadi wako katika masuala ya mtandao, tambulisha kila mtu mpya unayekutana naye angalau mtu mmoja mwingine.
- Epuka kuingilia maongezi ya watu walio kuwa katika kikundi cha watu wanne au zaidi. Unaweza kukaa pembeni na kuhakikisha kila mtu katika kundi hilo amesema kitu.
- Epuka kuingilia maongezi kwani unaweza kuwa unaharibu mazungumzo yao.
- Anzisha maongezi na watu ambao wamesimama au kukaa pekeyao, hii itawapa furaha kupata mtu wa kuongea nao hivyo kupelekea kwa watu hao kukupa habari muhimu ambazo katika hali ya kawaida si rahisi kuzipata.
- Jipe masaa 48 baada ya kukutana na mtu kwa mara ya kwanza kisha mtafute ili kumkumbusha kuhusu makutano yenu.
- Katika hafla za mitandao usijali kadi za biashara unazopata bali jali na tumia muda kutengeneza mahusiano machache yenye maana na manufaa.
Unapohudhuria hafla yoyote, hakikisha unaondoka ukiwa umejijengea heshima, na kutengeneza fursa ya kukutana tena na watu uliozungumza nao. Lengo sio kuuza bidhaa bali ni kutengeneza mahusiano ya muda mrefu.