Home BIASHARAUWEKEZAJI Epuka makosa haya unapowekeza

Epuka makosa haya unapowekeza

0 comment 150 views

Ukweli ni kwamba hakuna aliyekamilika na katika maisha lazima watu wapitie faida na hasara. Hasara hutokana na makosa ambayo mhusika hufanya kwa kujua au kutojua. Kuna baadhi ya makosa ambayo wawekezaji wengi  wa hisa wamekuwa wakiendelea kuyarudia. Habari njema ni kuwa makosa hayo yanaweza kuepukwa ili hali muwekezaji ana ufahamu.

Haya ni baadhi ya makosa na jinsi ya kuepukana nayo:

Ununuzi wa hisa katika biashara usiyoielewa

Mara nyingi wawekezaji huvutiwa kuwekeza katika tasnia inayotamba katika kipindi maalum hata kama wanajua kidogo, au hawajui lolote kuhusu biashara au kampuni husika wanayotaka kujihusisha nayo. Mara nyingi wanachojali ni faida watakayopata kwa kuwekeza katika biashara hiyo na sio uelewa mdogo walionao.

Iili kuepuka kuingia katika uwekezaji wenye hasara, ni vyema zaidi kuwekeza katika mambo ambayo una uelewa nayo. Hii itakusaidia kutathmini mambo yaliyopo, yanayoweza kutokea na hatari iliyopo ikiwa utawekeza.

Kutarajia mambo makubwa

Kuna umuhimu wa kufanya utafiti ili kujua kwanza historia ya hisa katika biashara husika na kujua hisa katika kampuni husika kupanda kwa asilimia ngapi, na hali iliyopo kwa washindani wa kampuni hiyo na mambo mingine ya msingi ni muhimu kuyajua. Ili iwe rahisi kufanya maamuzi na kuacha kusubiri muujiza utokee kwani kupanda na kushuka kwa hisa huwa hakutofautiani sana mwaka hadi mwaka.

Hivyo usiwekeze fedha ndogo ili hali unataka kupata fedha nyingi na usiwekeze hisa mahali ambapo historia ya hisa hairidhishi.

Kutumia fedha zenye matumizi mengine

Uwekezaji katika hisa ni hatari, hivyo ni muhimu kuwekeza fedha ambazo hazima matumizi ya haraka. Watu wengi huwekeza fedha ambazo hatari ikitokea basi na mfumo wao wa kifedha huathirika kwa kiasi kikubwa. Wekeza na fedha ambazo hazina matumizi mingine kwani hii itakusaidia kufanya maamuzi sahihi wakati unataka kufanya biashara.

Kutokuwa na uvumilivu

Mara nyingi wawekezaji huwekeza na kutaka matokeo moja kwa moja, jambo ambalo haliwezekani kwa sababu siku zote katika biashara huwa kuna mifumo inayoongoza ili kupata mafanikio. Mambo mbalimbali yanatakiwa kufanyika ikiwa ni pamoja na marekebisho ili kupata faida na hapo ndipo mwanahisa hunufaika. Uvumilivu ni muhimu kwa mtu yoyote anayetaka kuwekeza katika hisa.

Kujifunza uwekezaji sehemu zisizo sahihi

Sio kila habari unayoisikia ina ukweli ndani yake. Unaweza kusiki kuhusu mambo ya hisa na kufikiri faida hupatikana mara moja mjambo ambalo sio kweli. Kama muwekezaji unatakiwa kufanya utafiti ili kuweza kufanya maamuzi sahihi. Watu wengi wamewekeza katika hisa hewa na kutapeliwa kirahisi kutokana na kuamini kila kitu wanachosoma, kusikia au kuona katika vyombo vya habari.

Kufuata mkumbo

Mara nyingi watu husikia kuhusu uwekezaji pale unapokuwa umeenda vizuri. Ieleweke kuwa umaarufu wa uwekezaji hutangazwa tu pale ukishafanya vizuri. Hivyo badala ya kufuata watu unaweza kufanya utafiti na kujua mambo mengine muhimu ambayo yatakuhakikishia maendeleo. Sio kila uwekezaji una manufaa. Kitu kirahisi na kinachowezekana kwako kinaweza kuwa kigumu kwa watu wengine.

Kuwekeza kutokana na dhana moja

Wawekezaji wengi huwa hawajui kama wanafanya hivi, lakini mara nyingi wanaamini jambo fulani ni wazo zuri na litaleta faida na kuamua kuwekeza katika jambo hilo moja kwa moja. Ingekuwa ni rahisi hivyo basi kila mtu mwenye wazo zuri angeshakuwa tajiri.

Ni muhimu kwa wawekezaji kutambua kuwa inachukua zaidi ya wazo zuri kwa hisa fulani kuwa ni uwekezaji mzuri. Hivyo ni muhimu kujifunza hasa kutokana na makosa ili kufanya maamuzi sahihi na mazuri katika uwekezaji hasa wa hisa. Siku zote uelewa huleta urahisi wa kukabiliana na jambo lolote ikiwa faida au hasara imetokea.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter