Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla amezindua Hotel ya kisasa iliyopo ndani ya Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli kwaajili ya abiria na wageni wanaoingia na kutoka kwenye kituo hicho.
Hoteli hiyo ni ya ubia baina ya Halmashauri ya Ubungo na mwekezaji.
Akizindua hotel hiyo, RC Makalla ameelekeza hotel kuachwa ijiendeshe kibiashara ili kukuza mapato kwa Halmashauri ya Ubungo na kukemea watu kulala kwa “vimemo”.
Aidha, RC Makalla ametaka uendeshaji wa hoteli hiyo kuzingatia makubaliano ya kimkataba na uwazi katika kila kitu.
Hoteli hiyo ina idadi ya vyumba 38 ambavyo vikijaa vyote itaingiza Shilingi milioni 1.1 kwa siku, milioni 30 kwa mwezi na milioni 421 kwa mwaka ambapo Halmashauri ya Ubungo itachukuwa asilimia 60 ya mapato hayo na mwekezaji asilimia 40.
Pamoja na hayo RC Makalla ametumia uzinduzi huo kukemea wizi na uharibifu wa vifaa kwenye hoteli huku akielekeza Halmashauri ya Ubungo kutafuta wadau watakaoboresha mandhari ya nje ya kituo ikiwemo ujenzi wa bustani na sehemu za kupumzika kulingana na hadhi ya Kituo.