Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji Angellah Kairuki ameagiza Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuboresha huduma kwa wawekezaji kupitia mfumo wa huduma za mfumo wa mahala pamoja na mfumo wa kielektroniki. Kairuki pia ameitaka TIC kuunganisha kanda zote za kituo hicho na mfumo wa dirisha la uchakataji miradi (TIW) ili kurahisisha upatikanaji huduma kwa wawekezaji.
Waziri Kairuki ametoa maagizo hayo baada ya kuzungumza na maafisa wanaohusika na kutoa huduma ndani ya mfumo wa mahala ambapo walipata nafasi ya kujadiliana kuhusu namna ya kuboresha huduma hizo.
“Mfumo wa huduma za mahala pamoja ni mzuri sana, lakini tuhahitaji kuyafanyia kazi masuala kadhaa kwenye kila taasisi 11 zilizopo kwenye huduma za mahala pamoja ili kuondokana na changamoto ambazo zinachelewesha upatikanaji wa huduma za uwekezaji”. Amesema Kairuki.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Geoffrey Mwambe amesema serikali ikifanikiwa kuwezesha taasisi zote zinazohusika na huduma za mahala na vilevile kutoa huduma stahiki zinazohusu uwekezaji ndani ya ofisi za TIC, itakuwa ni hatua kubwa katika sekta ya uwekezaji.
“Taasisi zilizopo ndani ya mfumo wa mahala pamoja zinafanya kazi kubwa, tunachoomba sisi kama TIC ni kwamba huduma za taasisi hizo kwa wawekezaji zikamilike ndani ya TIC badala ya kwenda kwenye makao makuu ya ofisi hizo kufuata idhini ya vibali, leseni na vyeti husika kwa wawekezaji”. Amesema Mwambe.