Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linapaswa kuhakikisha kuwa, sekta hiyo inakua na kuwafikia wananchi wa kipato cha chini kwani mchango wake ni mkubwa katika kuchochea ukuaji wa viwanda. Majaliwa amesema hayo mjini Singida wakati akizindua mradi wa jengo la biashara na ofisi la Singidani Commercial Complex.
Katika uzinduzi huo, Majaliwa amewapongeza NHC kwa ujenzi huo na kudai kuwa, sekta ya nyumba mbali na kuchochea uchumi, pia ni chanzo cha ajira na husaidia kukuza uwekezaji wa viwanda vya vifaa vya ujenzi kama saruji, marumaru na nondo. Mbali na hayo, Waziri Mkuu pia ametoa wito kwa wadau mbalimbali kutizama sekta ya nyumba kama njia mojawapo ya kuleta maendeleo na kukuza uchumi kwa ujumla.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHC Felix Maagi amesema mradi huo ulianza mwaka 2015 na kukamilika Februari mwaka huu na umegharimu takribani Sh. 3.4 Bilioni. Jengo hilo la Singidani Commercial Complex linatarajiwa kuliingizia Shirika la Nyumba Sh. 420 Milioni kwa mwaka na hadi kufikia hivi sasa, asilimia 50 ya jengo hilo tayari limepangishwa.